Waziri Mkuu wa Ukraine yuko Berlin kutafuta msaada zaidi wa kijeshi

Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal alikaribishwa mjini Berlin na heshima ya kijeshi wakati nchi hiyo ikitafuta silaha zaidi nzito kwa ajili ya vita dhidi ya Urusi. Alikutana na Kansela Olaf Scholz, ambaye aliapa kuendelea kuisaidia Ukraine kijeshi, kisiasa na kifedha. Shmyhal aliandika kwenye Twitter kuwa walijadili jinsi ya kuimarisha uwezo wa ulinzi na msaada mwingine wa kina. Ujerumani imepeleka zana nzito nchini Ukraine kama vile vifaru 2,000 na vifaa vya kurushia makombora. Ujerumani pia itatuma mfumo wa ulinzi wa mashambulizi ya angani aina ya Iris-T. Hata hivyo, mahusiano kati ya Ukraine na Ujerumani yaliharibika kutokana na kucheleweshwa kupeleka vifaa vya kijeshi. Ujerumani pia imetangaza euro milioni 200 zaidi za kuwasaidia Waukraine ambao wamepoteza makazi yao nchini humo. Karibu watu milioni 7 wamekimbia makaazi yao lakini wamebaki katika nchi hiyo iliyoharibiwa kwa vita tangu uvamizi wa Urusi ulipoanza mwishoni mwa Februari.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii