Uamuzi kesi kupinga ushindi wa Ruto kutolewa mchana

Mahakama ya Juu ya Milimani ya Kenya inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu leo Jumatatu Septemba 5, 2022 saa sita mchana.

Kesi hiyo iliyofunguliwa na Raila Odinga aliyekuwa mgombea urais kupitia muungano wa Azimio na mgombea mwenza wake, Martha Karua kupinga matokeo ya urais yaliyotangazwa Agosti 15 na Mwenyekiti wa Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, Wafula Chebukati yaliyompa ushindi Rais mteule William Ruto.

Jana, Ruto ambaye ni Rais mteule wa Kenya alisema mambo yatakayotokea leo mahakamani wamemuachia Mungu na viongozi wa mahakama huku akiwataka Wakenya kumuombea Rais anayemaliza muda wake, Uhuru Kenyatta kusimamia kwa busara kipindi hicho cha mpito katika Taifa hilo.

Leo mchana, jopo la majaji saba linaloongozwa na Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Martha Koome na majaji Philomena Mbete Mwilu, Mohamed Ibrahim, Dk Smokin Wanjala, Njoki Susanna Ndung’u, Isaac Lenaola na William Ouko litatoa uamuzi wao kuhusu kesi ya hiyo ya kupinga ushindi wa rais mteule Ruto iliyofunguliwa na Odinga.

Uamuzi wa kesi hiyo utatoa uelekeo kama kama Ruto ataapishwa Septemba 13, 2022 kuwa Rais wa Kenya au kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga atapata fursa nyingine ya kuwania urais kama matokeo yatabatilishwa au atakwenda kustaafu siasa.

Majaji hao walijifungia kuandaa hukumu ya kesi hiyo tangu Ijumaa baada ya mawakili wa pande zote kuhitimisha uwasilishaji wa ripoti zao za mwisho katika jitihada za kushawishi majaji hao saba kukubaliana na misimamo yao katika kesi hiyo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii