Muqtada al-Sadr anaendelea na mapambano yake na wapinzani wake wa kisiasa nchini Iraq. Mhubiri huyo wa Kishia anatoa wito wa kuvunjwa kwa Bunge, miezi kumi tu baada ya kuchaguliwa kwake. Kwa siku kumi, wafuasi wake wamezuia shughuli za Bunge, wakipiga kambi karibu na jengo hilo. Na sasa anatoa wito kwa mahakama kuitisha uchaguzi wa mapema.
Kutokana na hatari kwamba makabiliano ya kisiasa yatageuka kuwa mapambano ya silaha na katika haraka ya kupata matokeo yaliyojadiliwa, wapinzani wa Muqtada al-Sadr walikuwa wamefungua mlango wa uchaguzi wa mapema. Haya ndiyo madai makuu ya kiongozi wa kidini wa Kishia ambaye alishindwa kuunda serikali. Lakini makubaliano bado hayajafikiwa.
Wapinzani wa Moqtada al-Sadr waliweka masharti ya kufanyika kwa uchaguzi huo. Sharti la kwanza kati ya mengine, lililokaririwa Jumatatu na Waziri Mkuu wa zamani Nouri al-Maliki, ni kurejelewa kwa vikao vya bunge. Ni Bunge hilo ambalo litapigia kura, kwa wingi unaohitajika, kuvunjika kwake. Lakini kiongozi huyo wa kidini anatoa wito kwa wafuasi wake kuendelea kukaa mbele ya jengo hilo ili kudumisha shinikizo kwa kambi pinzani na kuzuia uteuzi wa Waziri Mkuu asiyemtaka.
Akiwa amekabiliwa na mvutano huo, Muqtada al-Sadr sasa anaomba mahakama kulivunja Bunge. Anatoa wito kwa wabunge wake wa zamani na wafuasi wake kuwasilisha rufaa. Anahalalisha mtazamo wake kwa ukweli kwamba muda uliowekwa na Katiba wa uteuzi wa serikali umekwisha. Na kwa kufanya hivyo, Muqtada al-Sadr anaweka tarehe ya mwisho: Anaomba hadi mwishoni mwa wiki ijayo Bunge liwe limevunjwa.