Kocha msaidizi na mtaalamu wa viungo Simba, Karim Sbai amesema kwa muda wa wiki mbili aliokuwa kwenye kikosi hicho amefanikiwa katika maeneo mengi tofauti na alivyokuwa akitegemea na kwamba wapo tayari kwa vita ikiwamo pambano lao la watani dhidi ya Yanga. Kocha huyo, licha ya kuwakosa nyota watano waliokuwa katika timu ya taifa, Taifa Stars, akiwamo kipa Aishi Manula, bado anaamini siku saba za kukutana nao jijini Dar es Salaam zitamtosha kuwapika kabla ya kuvaana na Yanga kwenye Ngao ya Jamii.
Sbai alisema anajua cha kufanya na wachezaji watano walioshindwa kuwepo katika kambi hapa Misri kutokana na kuwepo katika majukumu ya Taifa Stars huku mmoja, Sadio Kanoute akishindwa kusafiri kutokana na masuala ya hati ya kusafiria.
“Wachezaji wote hao nimewapa programu maalumu ya kufanya ya mazoezi yao binafsi na nikifika Tanzania kabla ya kujiunga na wenzao nitawaangalia wamefikia wapi ili kufahamu kama kuna cha kuongeza au kupunguza,” alisema Sbai na kuongeza;
“Baada ya hapo ndio nitawapa ruhusa ya kujiunga na wenzao katika siku chache za maandalizi ya Simba Day pamoja na ile wiki moja ya kujiandaa kucheza na Yanga.”
Pamoja na Manula, wachezaji wa Simba waliokuwa katika kikosi cha Stars ni Mohammed Hussein, Kibu Denis, Mzamiru Yassin na Kennedy Juma.
Sbai alifichua pia kuwa wakati anafanya uamuzi wa kuja kufanya kazi Simba hakuamini kama atakuja kukutana na wachezaji wenye viwango kama waliopo kikosini humo wakati huu.