Morrison apewa wiki mbili Yanga

Morrison ameanza kazi rasmi Yanga na leo akiingia siku ya nne mazoezini, lakini kocha mmoja fundi wa mazoezi ameshtukia kitu kwa winga huyo Mghana kisha akamtengea siku 14 za kazi nzito.

Kocha aliyemshtukia BM33 ni Helmy Gueldich ambaye ni kocha wa mazoezi ya viungo aliyeangalia ubora wa mshambuliaji huyo kisha akagundua kwamba jamaa hakufuata sawasawa ratiba ya mazoezi waliyomtumia.

Helmy hata hivyo amesema Morrison yuko nusu fiti - nusu unga, lakini ndani ya wiki mbili tu atakuwa katika daraja lingine la ubora.

Kocha huyo alisema katika ratiba ya wiki ya kwanza Morrison atakuwa na kazi ngumu ambayo itamsaidia baadaye kurudisha ubora.

“Tulimpatia ratiba mapema kabla ya kujiunga alitakiwa kuifanya kwa ukamilifu lakini nimemuangalia naona hakuifuata sawasawa ila atakuwa sawa,” alisema Helmy ambaye bado anahitajika Chama cha Soka Tunisia.

“Ni mchezaji mzuri (Morrison) sio mbaya kwa hali aliyokuja nayo kitu kibaya angekuwa hajafuata kabisa lakini tuna muda wa kumrudisha katika mstari.”

Juzi Morrison alikimbizwa mazoezini Yanga akizunguka peke yake pembeni kisha akasimama na kulalamika akiongea kwa Kiswahili akisema: “Huyu jamaa anaiua huyu’ kauli ambayo mashabiki waliokuwa wakiangalia mazoezi hayo nje ya uzio walijikuta wakicheka huku wakishangilia.

Helmy ndiye aliyempunguza uzito beki Djuma Shaban kwa kilo tano kutoka 85 na kubaki na 79 hatua ambayo kocha Nasreddine Nabi amechekekelea akidai beki huyo atakuwa bora zaidi msimu ujao.

Wakati Helmy akimfua Morrison, kocha Nabi amefichua anajipanga kufanya kikao maalumu na winga huyo mwenye mbinu za kupangua ukuta.

Nabi alisema anaamini Morrison atakuwa ni mwiba mkali kwa wapinzani msimu ujao, lakini anataka kukaa naye wakiwa wawili tu kumpa mwelekeo wa maisha ndani ya kikosi hicho.

“Sifanyi hivi kwa Morrison peke yake nimeshazungumza na wengine wote ambao wamekuwa wakifika hapa. Ni vizuri akajua maisha yetu hapa na kitu gani tunakitaka kwake na vitu gani hatakiwi kuvifanya hapa,” alisema.

“Kila mmoja anampenda mchezaji mcheshi na hasa Morrison. Huyu ni mchezaji ambaye tumemsajili kwa mahitaji ya timu hasa malengo yetu kwa msimu unaokuja.”


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii