Jeshi la Polisi limemkamata mtu mmoja tuhuma mauaji ya Mwanafunzi wa Chuo UDSM

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limemkamata Gadi Daudi maarufu Tito Jeshi la Mtu mmoja (28) Mkazi wa Ubungo Riverside kwa tuhuma za kumuua Julius Fredrick (22) Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kumpora simu yake ya mkononi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya DSM, Muliro Jumanne amesema “Tukio hilo lilitokea 16/07/2022 majira ya saa kumi usiku huko eneo la karibu na hosteli za Magufuli Wilaya ya Ubungo Dar es Salaam baada ya kumvizia, kumshambulia na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili, kupora vitu vyake ikiwemo simu na kumsababishia kifo”

“Polisi DSM walipeleleza na 27/07/2022 walimkamata Sinza na alikiri kumuua Mwanafunzi huyo na kumpora na alikiri pia kufanya matukio kama ya unyang’anyi kwenye maeneo tofauti ya DSM, uchunguzi wa Polisi umebaini kuwa mtuhumiwa huyo ni mhalifu sugu ambaye amekuwa akifanya matukio ya kiuhalifu maeneo ya Mlimani city, Mwenge na Kawe, na aliwahi kushtakiwa kwa kesi ya unyang’anyi na kufungwa miaka 30 kuanzia July 06, 2020, na aliachiwa huru Aprili 2022 baada ya kukata rufaa”

“Aug 01,2022 Mtuhumiwa alikubali kuwapeleka Askari alipoficha silaha anazotumia katika uhalifu na simu ya marehemu aliyoipora katika vichaka vilivyopo eneo la katikati ya Mlimani city na Hostel za Magufuli na baada ya kufika eneo hilo alikurupuka na kuanza kukimbia, Askari walimzuia kwa risasi iliyomjeruhi kwenye paja la mguu, kuanguka chini na kukamatwa kisha kupelekwa hospitali kwa matibabu, eneo hilo Polisi imepata panga moja, sime, bisibisi na simu mbili za mkononi”

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii