Wanasheria mbalimbali wametoa maoni tofauti kuhusu kufukuzwa kazi kwa Meneja wa Shirika la Reli nchini (TRC) Kanda ya Dar es Salaam, Jonas Afumwisye huku baadhi yao wakionyesha nia ya kumpatia msaada wa kisheria.
Juzi, Afumwisye alipokea barua iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa ikimjulisha uamuzi wa shirika hilo wa kumfukuza kazi kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kuthibitishwa kwa makosa aliyoyafanya mwaka jana.
Baadhi ya makosa anayotuhumiwa kuyafanya ni kupinga juhudi za Serikali za kuanzisha tozo kwenye miamala ya simu na pia kupinga chanjo inayotolewa kwa wananchi kwa ajili ya magonjwa ya milipuko.
Kadogosa alibainisha makosa mengine kwenye barua hiyo kuwa ni kukashifu viongozi wakuu wa nchi, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kupitia makundi ya kijamii.
mawakili mbalimbali wamesema wako tayari kumsaidia Afumwisye kwa sababu hajatendewa haki katika kufukuzwa kwake na wengine wamebainisha kwamba alikiuka kanuni za utumishi wa umma.