Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imesisitiza wapangaji kuwa wazalendo na kulipia asilimia 10 ya kodi wanazokuwa wakilipa kwa wenyenyumba ili kulipia kodi ya pango.
Akiwa katika mafuzo ya wafanyabiashara juu ya mabadiliko ya sheria ya kodi mwaka 2022 wilayani Bariadi, Ofisa huduma na elimu mkuu kutoka TRA, Eugenia Mkumbo amesema kifungu cha 82(2) (a) cha sheria ya kodi kimefuta msamaha wa kodi kwa wapangaji binafsi hivyo kuwapa mamlaka wapangaji wote kuzuia kodi ya pango katika nyumba binafsi na zile za biashara ili kurahisisha ulipaji na ukusanyaji wa kodi ya pango.
"Kama umepanga chumba kiwe cha biashara au makazi unajukumu la kukata asilimia 10 na kuilipa TRA na mwenye nyumba utampelekea nakala ambayo inaonyesha umelipia kodi utaambatanisha na pesa iliyobaki unampa mwenye nyumba" amesema Eugenia.