Msemaji wa kundi la Taliban Zabihullah Mujahid amesema leo kuwa bado hawajaupata mwili wa aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda Ayman al-Zawahiri na wanaendelea na uchunguzi. Marekani ilisema ilimuuwa kiongozi al-Zawahiri katika shambulizi la kutokea angani mjini Kabul mwezi uliopita. Maafisa wa Marekani walisema jeshi la Marekani lilimuuwa kiongozi huyo wa al-Qaeda kwa kombora lililofyatuliwa na ndege isiyoruka na rubani wakati akiwa amesimama kwenye roshani ya chumba chake mwezi Julai. Mauaji hayo ni pigo kubwa kwa al-Qaeda tangu vikosi maalum vya Marekani vilipompiga risasi na kumuuwa Osama bin Laden zaidi ya muongo mmoja uliopita.