ISLAMABAD Polisi nchini Pakistan wamemfungulia mashitaka ya ugaidi waziri mkuu wa zamani Imran Khan na kusababisha kuuongeza mvutano wa kisiasa katika nchi hiyo. Hayo yameelezwa hii leo na maafisa nchini humo katika wakati ambapo Imran Khan akifanya mikutano mikubwa ya hadhara akipigania kurudi maradakani. Mashitaka hayo ya ugaidi yamefunguliwa kufuatia hotuba ya waziri mkuu huyo wa zamani aliyoitowa mjini Islamabad siku ya Jumamosi ambapo aliapa kuwashtaki maafisa wa polisi pamoja na jaji mmoja wa kike na kudai kwamba msaidizi wake wa karibu aliteswa baada ya kukamatwa. Chama cha Khan-Tehreek Insaf ambacho hivi sasa ni chama cha upinzani kilichapisha kwenye mtandao video ikionesha wafuasi wake wakiyazunguka makaazi ya Khan kwa lengo la kuwazuia polisi kutofika kwenye eneo hilo.Faisal Javed, Seneta na msemaji wa chama hicho amesema uhuru wa kweli unakaribia kufika Pakistan.Imeelezwa kwamba mamia ya wafuasi hao walikuwa katika eneo hilo hadi leo Jumatatu asubuhi. Chama hicho pia kimeonya kwamba kitafanya mikutano ya umma nchi nzima ikiwa Khan atakamatwa.