WAKENYA WAKUMBWA NA UKAME

Takriban Wakenya milioni moja kutoka maeneo kame wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame wa muda mrefu ambao umeathiri shughuli za kilimo.

Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Ukame (NDMA) jana ilisema kuwa watoto 884,464 ambao wapo chini ya umri wa miaka mitano, na akina mama 115, 725 ambao ni wajawazito, wanakabiliwa na utapiamlo kwa kukosa chakula cha kutosha mwilini.

Pia ufugaji umeathiriwa na ukame huo huku jamii za kuhamahama katika kaunti za Wajir, Marsabit, Isiolo na Mandera zikiathiriwa sana.

Kaunti hizo nne hazijapokea mvua kwa misimu minne mfululizo.

Vifo vya mifugo katika kaunti hizo, vilisababishwa na ukosefu wa malisho na maji kwa kuwa wanyama walilazimika kutembea umbali wa kilomita kadhaa kusaka maji na malisho.

“Kutokana na ukame huu, idadi ya raia ambao wanahitaji msaada wa vyakula inakadiriwa itapanda hadi watu milioni 4.35 kufikia Oktoba. Hii ni iwapo janga hili litaendelea kushuhudiwa nchini,” ikasema taarifa ya NDMA.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii