Ujumbe wa bunge la Marekani upo nchini Kenya kukutana na rais mteule na kiongozi wa upinzani ambaye anatarajiwa kuwasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi katika nchi hiyo yenye demokrasia imara zaidi katika ukanda wa Mashariki mwa Afrika. Balozi mpya wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman, amesema ujumbe huo unaoongozwa na Seneta Chris Coons pia utakutana na Rais wa Kenya anayeondoka Uhuru Kenyatta, ambaye mpaka sasa amesalia kimya tangu uchaguzi huo wa Agosti 9 uliokuwa wa amani kwa sehemu kubwa. Rais mteule William Ruto ni naibu rais wa Kenyatta, lakini viongozi hao wawili walitofautiana miaka kadhaa iliyopita, na Kenyatta katika uchaguzi huo alimuunga mkono kiongozi wa muda mrefu wa upinzani Raila Odinga. Odinga amesema anatafakari mbinu zote za kikatiba na kisheria kupinga matokeo ya uchaguzi huo.