Watunisia waunga mkono katiba mpya: matokeo ya mwisho

Matokeo ya mwisho ya kura ya maoni yenye utata inayoipa mamlaka makubwa ofisi ya Rais wa Tunisia Kais Saied yameonyesha kuwa ni asilimia 94.6 ya kura zilizounga mkono. Tume ya uchaguzi imesema wapiga kura waliidhinisha kwa wingi katiba mpya wakati ikitangaza matokeo ya mwisho ya kura hiyo ya maoni iliyofanywa Julai 25. Rais wa bodi ya tume hiyo Farouk Bouasker amewaambia waandishi habari kuwa katiba hiyo imeidhinishwa na watu milioni 2.6. Idadi ya wapiga kura waliojitokeza ilizingatiwa kuwa ya chini mno ikiwa ni asilimia 30.5. Kura hiyo ya maoni ilifanywa mwaka mmoja baada ya Saied kuwafuta kazi mawaziri na kulivunja bunge katika kile wapinzani wamesema ni mapinduzi. Licha ya idadi hiyo ya chini ya wapiga kura, hatua ya Saied dhidi ya mfumo ambao uliibuka baada ya kuangushwa kwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Zine El Abidine Ben Ali mwaka wa 2011 imekaribishwa na Watunisia wengi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii