Lula, Flavio Bolsonaro wakabana koo duru ya pili Brazil

Rais wa Brazil Lula da Silva na mpinzani wake Flavio Bolsonaro wako sare katika kura ya maoni, kila mmoja akiungwa mkono kwa asilimia 50. Wanajiandaa kuchuana katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais Oktoba 25.

Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Brazil Oktoba 25, hakuna mgombea anayeonekana kuwa na nafasi ya wazi ya kushinda. Rais wa sasa mwenye mrengo wa kushoto, Luiz Inacio Lula da Silva, na mpinzani wake mwenye mrengo wa kulia, Flavio Bolsonaro, wako sare katika kura mpya ya maoni.

Utafiti wa taasisi ya PoderData unaonyesha kila mgombea akiungwa mkono kwa asilimia 50. Matokeo hayo yamekuja baada ya kura tatu za maoni za wiki iliyopita kuonyesha Bolsonaro akiwa mbele kwa tofauti ndogo.

Ushindani huo unaweza kuwa mkali kama ule wa mwaka 2022, wakati Lula alipomshinda baba yake Flavio, Jair Bolsonaro, kwa kupata asilimia 50.9 ya kura. Jair Bolsonaro baadaye alifungwa kwa kujaribu kufanya mapinduzi ili aendelee kubaki madarakani.
Flavio Bolsonaro alishinda kwa kushtukiza duru ya kwanza ya uchaguzi Oktoba 4, akipata asilimia 47 ya kura. Kambi yake ya mrengo wa kulia pia iliongeza viti vingi bungeni, huku vyama vya siasa vya mrengo wa kati vikipoteza nafasi.

Katika wiki iliyofuata, baadhi ya kura za maoni zilionyesha Bolsonaro akimzidi Lula kwa hadi pointi sita za asilimia. Hata hivyo, Lula ameimarisha kampeni yake kupitia mikutano mikubwa nchini kote na shughuli kwenye mitandao ya kijamii. Bolsonaro, ambaye alikuwa amepunguza kampeni za mitaani kutokana na kuongoza kwenye kura za maoni, sasa ameanza tena kuhamasisha mikutano mikubwa ya wafuasi wake.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii