ICC yashinda Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo 2026

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na maofisa wake wameshinda Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo ya mwaka 2026, inayotolewa na Bunge la Ulaya, ikimshinda Tundu Lissu na mabinti wawili wa Iran.

Tuzo hiyo inatambua juhudi za kutetea haki za binadamu na uhuru wa msingi. ICC, yenye makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi, inachunguza na kushtaki wahusika wa uhalifu mkubwa wa kimataifa, ukiwemo uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari.

Mahakama hiyo imechaguliwa kuwa mshindi mbele ya wagombea wengine wawili waliofika hatua ya mwisho, ambao ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, na dada wawili wa Iran, Taraneh na Romina Rahimi.

Ushindi huo umetangazwa wakati ICC ikikabiliwa na vikwazo vya Marekani dhidi ya taasisi hiyo na baadhi ya maofisa wake.

Mahakama hiyo imesema vikwazo hivyo vinatishia uhuru wake wa kimahakama na imezitaka nchi mbalimbali kuunga mkono shughuli zake.

Tuzo ya Sakharov hutolewa kila mwaka na Bunge la Ulaya, kwa watu au taasisi zinazotambuliwa kwa juhudi zao za kutetea haki za binadamu na uhuru wa msingi. Ilianzishwa mwaka 1988 na kupewa jina la mwanasayansi na mwanaharakati wa upinzani wa Kisovieti, Andrei Sakharov.

Sherehe ya kukabidhi tuzo hiyo inatarajiwa kufanyika mjini Strasbourg, Ufaransa, Desemba 16, mwaka huu.

Aidha, Lissu alikuwa miongoni mwa waliofika hatua ya tatu bora katika kuwania tuzo hiyo, akitambuliwa kutokana na harakati zake za kutetea demokrasia, mageuzi ya katiba na uchaguzi huru na wa haki.

Lissu anatuhumiwa kwa uhaini akiwa gerezani tangu Aprili 2025, alipokamatwa na sasa anasubiri hukumu ya tuhuma hizo inayotarajiwa kutolewa Novemba 06, 2026.

Wagombea wengine waliofika hatua ya mwisho walikuwa dada wa Iran, Taraneh na Romina Rahimi, waliotajwa katika uteuzi huo kwa niaba ya watu wanaokabiliwa na mateso nchini Iran.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii