Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameitaka jamii kuanzisha kampeni ya nyumba kwa nyumba kuhamasisha wananchi kujiunga na mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa na kupanua upatikanaji wa huduma za matibabu.
Chalamila ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Bima ya Afya kwa Wote katika mkoa huo, akisema Serikali imeupa kipaumbele mpango huo ili kuwasaidia Watanzania kupata huduma za matibabu bila kukabiliwa na gharama kubwa wanapougua.
Amesema bima hiyo, inayogharimu Sh150,000 kwa mwaka, inahusisha mtu mmoja pamoja na familia yake yenye watu watano, hivyo kuwasaidia kupata huduma za afya kulingana na mafao yaliyoainishwa katika mpango huo.
Ameeleza kuwa watu wanaweza kukumbwa na magonjwa wakati hawana fedha za kugharamia matibabu, hivyo kuwa na bima kunaweza kupunguza mzigo wa gharama za huduma za afya.
Mkuu huyo wa mkoa amewahimiza wananchi wa makundi mbalimbali kujiunga na mpango huo bila kujali kiwango cha kipato, akitaja magonjwa yasiyoambukiza, yakiwamo kisukari na shinikizo la juu la damu, kuwa miongoni mwa yanayoweza kuhitaji gharama kubwa za matibabu.
Amesisitiza umuhimu wa kuanza utekelezaji wa mpango huo mara moja ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma zinazotolewa.
Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa Kinondoni, Fidelis Steven, amesema kaya 5,095 katika Mkoa wa Dar es Salaam zimejisajili katika mfumo huo wa Bima ya Afya kwa Wote.
Steven amewahimiza wananchi wengine kujitokeza kujiunga na mpango huo ili kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za matibabu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema ni muhimu kuhakikisha mfumo huo unawafikia Watanzania wote ili kupunguza changamoto wanazokabiliana nazo wanapohitaji huduma za afya.