nyongeza ya mshahara ni jambo ambalo baadhi ya watumishi wa umma wamekuwa wakijiuliza tangu juzi, baada ya Serikali kuweka nyongeza ya mishahara huku baadhi wakiambulia Sh20,000!
Hilo limefanya watumishi wa umma kulipuka kupitia mitandao ya kijamii wakihoji kama ni nyongeza ya mshahara iliyotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan au nyongeza ya kisheria (annual increment) inayopaswa kuongezwa kila mwaka.
Mtumishi mmoja wa Serikali ambaye anapata mshahara unaokaribia Sh2 milioni, alisema katika akaunti yake amekuta ameongezewa Sh18,000 ambayo anasema haitoshi kufanya ununuzi sokoni ukilinganisha na miaka waliyosubiri nyongeza.
Katibu Mkuu, Utumishi na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro, alisema miaka yote utaratibu unaotumika ni huo huo, lengo likiwa kupunguza pengo kati ya yule wa chini na wa juu.
“Hizi asilimia haziwi constant (hazifanani kwa wote), zinapanda na kushuka, wa chini zitapanda na kadiri zinavyokwenda juu zinapungua na lengo la Serikali ni kuwainua wa chini wapande juu. Unapo boost (kumuinua) chini wale wa juu inapungua,” alisema Dk Ndumbaro huku akiongeza watatoa ufafanuzi wiki ijayo.
Mitandao yalipuka
Katika mitandao ya kijamii ni kama kumelipuka bomu kutokana na nyongeza hiyo kutokidhi matarajio ya baadhi ya watumishi, huku wakisema zamani nyongeza ilionekana na haikuhitaji tafsiri.
Katika kuthibitisha suala hilo limekuwa kaa la moto kwa Serikali huku baadhi ya watu wakituma hata vibonzo kuonyesha mshangao wa kile walichokiona kwenye akaunti zao, juzi usiku baada ya kelele kuanza kusambaa mitandaoni, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alijitokeza hadharani akiwasihi watumishi kutulia.
Msigwa kupitia ukurasa wa Twitter saa 4:08 usiku aliandika ujumbe usemao “Ndugu wafanyakazi naomba tutulie. Serikali itatoa ufafanuzi kuhusu nyongeza ya mishahara iliyotokea katika mishahara ya mwezi Julai 2022.”
Wakati Msigwa akisema hivyo, Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya alisema ni kweli yapo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wakilalamikia nyongeza hiyo ya mishahara iliyowekwa na Serikali.
“Taarifa hizi za nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa sekta ya umma, tumeipokea tumeifuatilia, ni kweli haijakaa vizuri na tutalizungumzia suala hilo wiki ijayo tutakapokuwa kwenye kikao chetu Dodoma,”alisema Nyamhokya.
“Tunaomba watumishi watulie tutakaa pamoja na Serikali halafu tutawaambia kwa kiwango gani watumishi hatujaridhika na aina ya uongezaji mishahara ilivyofanyika,”.Mei 14 mwaka huu, Rais Samia aliridhia mapendekezo ya kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma, ikiwamo kima cha chini kwa asilimia 23.3 ambapo Sh1.59 trilioni zitatumika katika nyongeza hiyo, na imeanza katika mshahara wa Julai.
Walichosema wafanyakazi
Kuanzia juzi jioni na jana kulitokea mtikisiko katika mitandao ya kijamii, hususan Twitter, Facebook, Instagram na makundi sogozi ya Whatsapp, baada ya wafanyakazi kuingiziwa mishahara ambayo haikuwa na nyongeza waliyoitegemea.
Mwalimu mwandamizi mkoani Rukwa, alidai mwalimu mwenye ngazi ya mshahara TGTS B ambaye mshahara ghafi ni Sh484,000 kwa mwezi ameongezewa Sh65,000 wakati wa TGTS H anayelipwa Sh2.1 milioni ameongezewa Sh25,000.
“Nyongeza hii ni kabla ya makato yote ya kisheria. Yaani anachopata mtu ni kidogo na unaweza usione kama kuna nyongeza yoyote. Hatukutarajia haya kabisa. Ni kama tumepigwa na kitu kizito kichwani,” alidai mwalimu huyo.
Mtumishi mwingine ambaye ni mwalimu wa sekondari mkoani Mtwara anayepata mshahara unaokaribia Sh800,000 alisema amekuta nyongeza ya Sh30,000, “yaani sijui hii imekaaje ila tumepigwa na kitu kizito.
“Mfano mimi niko kwenye daraja D nimeongezewa Sh55,000 na hii inakutana na makato yote ya bima, Paye (kodi ya mapato), CWT (chama cha walimu), hifadhi ya jamii kwa hiyo hadi mwisho nimekuta kwenye akaunti kama Sh30,000,” alisema na kuongeza:
“Sasa fikiria, hatujaongezewa mishahara karibu miaka saba, tulitarajia nyongeza ianzie Sh80,000 na kuendelea ambayo itaingia kwenye akaunti, lakini kweli miaka saba tunakuja kuongezewa Sh20,000?”
Kwa upande wake, askari mmoja wa Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, alisema kilichotokea katika nyongeza ya mishahara ni tofauti na matarajio ya wengi hadi wanafikia mahali na kuwaza pengine kuna tatizo katika ukokotoaji wa hesabu.
“Rais Mkapa aliboresha mishahara kwa kiasi kikubwa. Yeye ndiye aliwafanya askari waweze kukopesheka magari. Wakati anaingia madarakani alikuta posho ya polisi ni Sh50,000 kwa mwezi, lakini mpaka anaondoka ilikuwa Sh300,000,” alidai.
“Yeye alikaa miaka 10 lakini nyongeza unaiona na inashikika. Kipindi hiki tumesubiri kwa miaka saba halafu kilicholetwa eti mpaka kifafanuliwe, ulisikia wapi bwana mwandishi. Nyongeza inatakiwa ijionyeshe yenyewe,” alihoji.
Hata hivyo, mwalimu wa shule ya sekondari Mawenzi ya mjini Moshi, Wilfred Mauki alisema baadhi ya watumishi wamechanganya kati ya ongezeko la kila mwaka la mshahara na ongezeko linalozingatia hali ya uchumi wa nchi.
“Wameshindwa kutofautisha kati ya annual increment (ongezeko la kisheria la kila mwaka) na hii nyongeza aliyoitangaza Rais. Hii sio annual increment, tungepewa hii ndio ungekuta kuna ongezeko labda la Sh100,000 kwa mwezi,” alisema Mauki.
Kwa upande wake, mwalimu Stephen Mnguto wa Ngorongoro alisita kutoa maoni yake, akisema anataka kufanya utafiti mdogo kujua fomula iliyotumika katika nyongeza hiyo hadi mmoja aongezewe Sh20,000 na mwingine Sh65,000.