Serikali ya Mali imetaka ufafanuzi juu ya uhusiano uliopo kati ya serikali ya Ujerumani na wanajeshi 49 wa Ivory Coast waliokamatwa mjini Bamako wiki iliyopita. Wanajeshi hao walizuiliwa tarehe 9 Julai, wakituhumiwa kuingia nchini Mali kinyume cha sheria, kuwa mamluki na kuyumbisha usalama wa serikali ya Bamako. Wizara ya ulinzi ya Ujerumani hata hivyo inasema kuwa wanajeshi wa Ivory Coast wamekuwa wakiilinda kambi ya Umoja wa Mataifa kwenye uwanja wa ndege wa Bamako tangu mwaka 2019, huku serikali ya Mali ikifahamu kuwepo kwao. Ingawa kulingana na kamandi ya jeshi la Ujerumani, shirika la ndege la nchini Mali la SAS ni mshirika wa Ujerumani, kamandi hiyo imesema haina mkataba na wanajeshi hao waliokamatwa. Umoja wa Mataifa umeelezea uwezekano kuwa Ivory Coast imewapeleka wanajeshi hao chini ya mkataba na mshirika wa ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa, MINUSMA.