Mkuu wa jeshi la Israel azuru Morocco kwa mara ya kwanza

Mkuu wa jeshi la Israel Aviv Kohavi anaendelea na ziara yake ya siku tatu nchini Morocco ambapo anatarajiwa kufanya mikutano na maafisa wandamizi wa ulinzi wa vyeo vya juu huku ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ukitanuka kufuatia kurejeshwa kwa mahusiano ya kawaida ya kidiplomsia. Kohavi aliwasili jana mjini Rabat katika ziara ya kwanza rasmi kuwahi kufanywa na mkuu wa mejeshi ya Israel katika nchi hiyo ya utawala wa kifalme Afrika Kaskazini. Msemaji wa Israel amesema Kohavi atakutana na mjumbe wa waziri wa Morocco anayehusika na usimamizi wa masuala ya ulinzi Abdellatif Loudiyi pamoja na Inspekta Jenerali wa majeshi ya Morocco luteni Jenerali Belkhir El Farouk na maafisa wa vyeo vya juu wa ulinzi. Morocco ilikata uhusiano na Israel mnamo 2000 kufuatia kuzuka kwa vita vya pili vya Palestina vya intifada lakini ikarejesha mahusiano miongo miwili baadaye katika mkataba ulioshuhudia Marekani ikiutambua uhuru na mamlaka ya Morocco juu ya eneo la Sahara Magharibi linalozozaniwa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii