IMF yaipa Tanzania mkopo wa dola bilioni moja

Shirika la Fedha la Kimataifa IMF limesema limeipa Tanzania mkopo wa dola bilioni 1.046 utakaotolewa katika kipindi cha miezi 40, kwa lengo la kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na athari za vita vya Ukraine. Taarifa ya shirika hilo imesema athari za vita vya Ukraine vinakwamisha juhudi za kuondokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la ugonjwa wa Covid-19, na hivyo kudumaza maendeleo na kuongeza changamoto za mageuzi yanayonuiwa kuiwezesha kutumia kikamilifu uwezo wake kiuchumi. Kutokana na hayo, wataalamu wa IMF wanaamini Tanzania itahitaji kufanya mageuzi na itumie uwezo wake kiuchumi. Mradi huo uliotangazwa jana Jumatatu unatakiwa kusaidia mageuzi katika masuala ya fedha kuimarisha uthabiti wa kifedha wa Tanzania, kufanya uwekezaji wa umma na kuisaidia sekta binafsi. Tanzania itapokea mara moja dola milioni 151.7. Ilikuwa tayari imepokea mkopo wa dola milioni 567 mwishoni mwa mwaka uliopita kushughulikia mahitaji yake muhimu ya dharura wakati janga la Covid-19 lilipokwamisha maendeleo ya kiuchumi, hususan katika sekta ya utalii.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii