Taiwan imesema imetuma ndege mbili kuziteka ndege za kivita za China karibu na kisiwa hicho chenye utawala wake wenyewe. Taipei imesema ndege 22 kati ya 27 za China zilivuuka mstari wa Lango Bahari la Taiwan, na kwamba ilituma ndege za ulinzi wa doria na kuwacha mitambo yake ya ulinzi katika kuzifuatilia ndege za China. Hatua hii inakuja siku moja tu kabla ya Jeshi la Ukombozi la China kuanza mazoezi matano ya kina kuzunguka kisiwa hicho. Luteka hilo la China litafanyika pande sita tafauti kuzunguka kisiwa kizima cha Taiwan. China inakichukulia kisiwa hicho kuwa ni sehemu ya mamlaka yake. Maafisa wa mataifa ya Magharibi wameelezea khofu zao kwamba mvutano wa kijeshi nchini Taiwan unatokea sambamba na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Hatua ya China inakuja baada ya Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi, kuitembelea Taiwan, akiwa afisa wa juu kabisa kufanya ziara rasmi kwenye kisiwa hicho kwa miaka 25 iliyopita.