Zikiwa zimebaki siku 10 kabla ya Simba na Yanga kukutana kwenye mchezo wa ufunguzi wa ligi wa Ngao ya Jamii, Agosti 13 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kocha wa Simba, Zoran Maki amekisuka kikosi chake, kisha akasema sasa kipo tayari kwa ajili ya mashindano.
Simba ambayo ipo mjini hapa ilipoweka kambi ya wiki tatu sasa, imekuwa ikijifua na kujiweka fiti katika mambo mbalimbali ya uwanjani ikiwamo utimamu wa miili.
Zoran amesema katika utimamu wa miili wachezaji wapo sawa na upande wa mbinu wamepokea vizuri maelekezo na kwamba, ameliona hilo hata katika mechi nne za kirafiki walizocheza na kama kuna marekebisho machache, basi ni yale madogo ambayo watayajenga wakiwa Dar.
Amesema kazi kubwa aliyokuwa nayo ni kuhakikisha wachezaji wanaonyesha mchezo bora katika kilele cha Siku ya Simba (Simba Day), Jumatatu ijayo, kwani mbali ya kushinda anataka kuwaona mastaa hao wanacheza soka la kuvutia na la haraka muda wote.
“Baada ya hapo tutakuwa na siku chache kufanya maandalizi mengine kabla ya kucheza mechi ya ufunguzi wa msimu dhidi ya Yanga na jinsi ambavyo tumefanya maandalizi, naamini tunakwenda kushinda na kuanza msimu vizuri tukiwa na taji la kwanza,” alisema Zoran.
“Mechi yoyote ya dabi katika nchi zote nilizopita ni ngumu, lakini maandalizi tuliyofanya huku Misri, wachezaji walivyoimarika tofauti na nilivyowakuta, usajili wa wachezaji wapya pamoja na ubora wa kikosi naamini tunakwenda kushinda.