India imethibitisha kifo cha kwanza cha mgonjwa wa homa ya nyani hapo jana. Wizara ya Afya katika jimbo la kusini la Kerala imesema mgonjwa aliyefariki alikuwa kijana wa miaka 22. Uhispania iliripoti vifo viwili vya aina hiyo wiki iliyopita, huku kifo kimoja kikitajwa kutokea Brazil na chengine nchini Peru. Tarehe 23 Julai, Shirika la Afya Duniani, WHO, iliutangaza ugonjwa huo kuwa dharura ya kilimwengu. Shirika hilo limeripoti kugundulika wagonjwa 18,000 kutoka nchi 78 nje ya bara la Afrika, ambako ugonjwa huo umeenea zamani. Kwa mujibu wa WHO, virusi vya ugonjwa huo husambazwa kutoka kwa wanyama. Miongoni mwa ishara zake ni homa kali, maumivu ya misuli na majipu. Ingawa chanjo zake zipo, kuna tatizo kubwa la usambazaji wake.