Kambi ya Simba mambo ni moto.

Kambi ya Simba inaendelea kunoga, huku kocha Zoran Maki akisaliwa na wiki kama moja tu kukamilisha programu zake kabla ya kuja kuwasha mitambo katika tamasha la Simba Day kisha kuliamsha dude mbele ya watani wao kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 13.

 Simba iliondoka nchini Julai 14 na kuanza mazoezi siku iliyofuata katika hoteli ya kishua ya Mercure Ismailia Forsan Island na hadi kufika leo imefikisha siku 13 za kutengeneza kikosi na imebakiza siku nane kati ya 21 zilizopangwa kwa ajili ya kambi hiyo iliyopo chini ya kocha Zoran.

Katika siku 13 za kujifua, Zoran amezitumia kujenga utimamu wa miili ya wachezaji, kuongeza pumzi na kutambulisha mbinu mbalimbali watakazozitumia kwa msimu ujao na kuwafanya wachezaji kucheza kwa kuelewana na kutengeneza mifumo zaidi ya miwili tofauti.

Ili kuhakikisha anajua maendeleo ya timu, Zoran alicheza mechi mbili za kirafiki, ya kwanza dhidi ya Ismaily na kutoka sare ya 1-1 kisha kuifumua Al Akhdood kwa mabao 6-0 na jana ilikuwa uwanjani tena kwa mchezo wa tatu dhidi ya Haras El Hadood.

Katika mechi mbili za awali, wachezaji Patrick Phiri, Augustine Okrah, Mohamed Ouattara, Pape Sakho, Meddie Kagere na Clatous Chama walitakata na kumfurahisha kocha, ambaye kwa sasa amekabidhiwa panga na kuwakata nyota wa kigeni waliozidi ili kubakiza 12 wanaotakiwa na kanuni.

“Nina furaha na tulichokifanya hadi sasa, maendeleo yanaonekana kwa mchezaji mmoja mmoja na timu nzima kwa ujumla, tumebakiza siku chache hapa ambazo tutazitumia kumalizia maandalizi ya msimu ujao na baada ya hapo naamini tutakuwa tayari kwa mapambano,” alisema Zoran.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii