Kocha mkuu wa Simba, Zoran Maki amewaambia wachezaji kuwa atakayefanya vizuri ndiye atakayepata nafasi ya kucheza bila kujali ukubwa wa majina.
Kauli hiyo ni kama amewatangazia kwamba kikosi chake kinaanza upyaa chini yake ili kurejesha ubabe wao Ligi Kuu Bara.
Hayo yamesemwa na kocha msaidizi wa timu hiyo ambayo imepiga kambi yake nchini Misri, Seleman Matola akielezea namna ambavyo wanaendelea na maandalizi.
Matola alisema Zoran amekuwa kama kocha mzoefu na mwenyeji ndani ya kikosi hicho kwani hata falsafa ya ufundishaji inaendana na mwongozo wa klabu. “Kocha amewaambia (wachezaji) hataangalia nani alikuwepo msimu uliopita na alifanya nini. Mchezaji atakayefanya vizuri ndiye atakayepata nafasi ya kucheza hivyo kila mmoja anajituma,” alisema Matola.
“Ukiangalia ushindani ndani ya timu ni mkubwa kila namba ina mtu na mtu, hivyo hapo ni kila mmoja kujituma na kuongeza juhudi zaidi maana wale ambao tuliona msimu uliopita hawakupata nafasi kubwa kucheza wanajituma zaidi na wale wengine hivyo hivyo.”
Kuhusu maendeleo ya kambi Matola alisema: “Ukiangalia tulivyoanza na tunavyoendelea kuna mapokeo makubwa kwa wachezaji, tunaamini ushindani utaongezeka.”