Asilimia 67.2 wakazi Dar wana uzito kupita kiasi

Asilimia 67.2 ya wakazi wa Dar es Salaam wana uzito kupita kiasi huku wengi wao wakiwa ni wanywaji wa pombe wa mara kwa mara, utafiti wa hivi karibuni umeonyesha.

 Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Pedro Pallangyo alisema utafiti huo ulifanyika mwaka 2020 ukihusisha watu 6,691.

Alisema utafiti huo mkubwa zaidi kuwahi kufanyika nchini, ulihusisha wanawake na wanaume ambapo wanawake walionekana kuwa na uzito uliokithiri zaidi ikilinganishwa na wanaume.

Dk Pedro alisema utafiti huo uliolenga kuangalia suala la uzito jijini Dar es Salaam ulihusisha watu wenye umri wa wastani wa miaka 43.1 ambao asilimia 54.2 walikuwa ni wanaume.

“Tuliangalia aina ya ulaji wa watu, ufanyaji wa mazoezi, unywaji wa maji na uvutaji wa sigara,” alisema.

Alisema kwenye suala la ulaji, waligundua watu wanaotumia vyakula nje ya nyumbani hasa wakinunua migahawani, walionekana kuwa na uzito mkubwa ikilinganishwa na wale wanaobeba vyakula kutokea nyumbani.


“Kikubwa ni kwamba wanakula si kwa sababu wanakosa mlo, ila kwa sababu hawana nidhamu ya muda wa kula, wanakula muda wowote na wanaishia kula chakula ambacho si kizuri kiafya.

“Mfano ingekuwa mtu nyumbani kwake angetumia chai ya rangi au maziwa akatumia na mkate asubuhi, kwa sababu ya ratiba zake akaruka mlo wa mchana, ataishia kula chipsi mayai na vingine lakini si kwa sababu asubuhi hakula. Atanunua tena kitu kingine na kwa sababu kila kitu kimechelewa, hata mlo wa usiku atakula amechelewa, hivi vyote vinachangia kupata uzito mkubwa,” alisema.

Pia Dk Pedro alisema waliangalia mwenendo wa ulaji wa mbogamboga na matunda kwa siku kulingana na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO), ambapo walibaini wale waliokuwa na ulaji mdogo kuliko inavyopaswa walikuwa kwenye hatari zaidi ya kupata uzito uliokithiri.

Aliwataja wenye shinikizo la juu la damu, wanywaji wa pombe na watu wasiozingatia unywaji wa maji kuingia kwenye hatari hiyo ya uzito uliokithiri kulingana na utafiti wao.

Kuhusu ufanyaji wa mazoezi, Dk Pedro alisema asilimia 88.3 ya watu wote waliofanyiwa utafiti hawakuwa na tabia ya kushughulisha mwili walau nusu saa kwa siku tano kwa wiki.

Alisema mapendekezo ya WHO yanaelekeza mtu kufanya mazoezi kwa saa mbili na nusu kwa siku tano kwa wiki.

Dk Pedro alisema kupitia utafiti huo, walishauri Wizara ya Afya na Idara ya Afya ya Jamii kuja na mkakati wenye kuwezesha wananchi kupata elimu juu ya madhara ya ulaji usiofaa na umuhimu wa kufanya mazoezi.

Ofisa lishe mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Fatma Mwasora alisema ili kukabiliana na uzito uliokithiri na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni muhimu kupunguza vyakula vya mafuta na wanga.

“Ale mbogamboga kwa wigi, asile ugali, wali, mkate kwa wingi, asiruke mlo. Mtu ahakikishe anakula milo mitatu kwa siku na ahakikishe anafanya mazoezi hata kama hapati muda ofisini, anaweza kunyanyuka na kutembea kidogo,” alisema.

Kulingana na takwimu za WHO watu milioni 41 sawa na asilimia 71 hupoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na watu milioni 15 hufariki dunia wakiwa na umri kati ya 30 na 69.

Kwa hapa nchini asilimia 27 ya vifo vinavyotokea husababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza WHO.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii