Wakenya wakosa kulipa mikopo ya Sh483 bilioni

Gharama ya maisha inapozidi kulemea Wakenya, imebainika kuwa wengi wamekosa kulipa mikopo yao huku kiasi cha madeni wanayodaiwa kikigonga Sh483 bilioni kufikia mwezi Mei 2022.

Takwimu za Benki Kuu ya Kenya (CBK) zinaonyesha kuwa mikopo ambayo haijalipwa imekuwa ikipanda tangu Desemba 2021 wakati deni lilikuwa Sh426 bilioni.

Mnamo Mei, deni la Wakenya lilipanda hadi Sh483.8 bilioni, hali ambayo inaashiria kuwa haki inazidi kuwa ngumu kwa benki na asasi zinazokopa fedha na kuchangia kukua kwa uchumi.

Hata hivyo, imebainika kuwa Wakenya wengi sasa wanakimbilia mikopo ili kujikimu na kuwekeza katika biashara zao ambazo pia hazifanyi vizuri kutokana na athari ya janga la virusi vya corona na mfumko wa kiuchumi.

Mnamo Mei 2021, benki zilitoa mkopo wa Sh361 bilioni na mwaka huu mikopo ambayo ilitolewa kwa kampuni zinazohimili sekta za kibinafsi ni Sh3.44 trilioni.

Hii ilikuwa kiasi cha juu ikilinganishwa na Sh181 bilioni benki zilitoa kama mkopo kwa wakati sawa na huo mnamo Mei, 2020.

Benki nyingi nchini ndizo zimetikiswa na wanaokopa kukosa kurudisha fedha zao, kwa kuwa maisha ya Wakenya wengi yalisambaratishwa na ujio wa virusi vya corona ambao ulisababisha kutokomea kwa ajira.

Aidha bei ya bidhaa za kimsingi kama mafuta zimepanda na kuwaumiza Wakenya zaidi hasa katika kujikimu, kuimarisha biashara zao na kulipa mikopo yao.

Sekta za utengenezaji bidhaa, mauzo ya makazi, wafanyabiashara wa kibinafsi ambao ndio hukopa sana pesa, ndio wamelemewa kuyalipa madeni yao.

Shirika la Kimataifa la Kifedha (IMF) wiki jana lilionya kuwa uchumi wa taifa huenda hautakua na kupitisha asilimia 10 na kuzishauri benki kuwa sasa lazima zimakinike na kutafakari zaidi kabla ya kutoa mkopo.

“Biashara ndogondogo zinalemewa sana kulipa mikopo lakini zinatekeleza wajibu muhimu katika ukuuaji wa kiuchumi. Itachukua muda sana kabla ya biashara zao kurejelewa vyema ili waanze kulipa mikopo yao,” ikasema IMF.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Muungano wa Benki Nchini (KBA) Habil Olaka mnamo Mei 2021 alisema kuwa benki zilifanya vyema na kupata faida ya Sh143.71 bilioni baada ya ushuru kutokana na malipo ya mikopo iliyokuwa imechukuliwa na wafanyabiashara.

“Japo wengi wao walipata hasara mnamo 2020, walijitahidi na biashara zao zikaimarika ndiposa kulikuwa na mabadiliko kuhusu ulipaji wa mikopo,” akasema Bw Olaka.

Uchumi wa Kenya ulipanda kwa asilimia 7.5 kufuatia hatua ya serikali ya kufungua nchi na uchumi baada ya athari hasi ya janga la corona lililosababisha kuwekwa kwa kafyu mara kwa mara.

Pia hatua ya serikali kuwekeza fedha katika sekta mbalimbali na kupunguza ushuru ilichangia kuimarika kwa uchumi wa nchi baada ya janga la corona.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii