Wavenezuela" Chebukati abaki kimya".

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Jumatatu iliendelea kubaki kimya kwa siku ya pili mfululizo, baada ya Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kutoa taarifa ndefu ikiilaumu kwa kutoeleza ukweli kuhusu raia watatu wa Venezuela waliokamatwa katika uwanja wa ndege wa JKIA.

Raia hao watatu walikamatwa na maafisa wa DCI wakiwa na vibandiko vya vifaa vya kuendeshea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 mara tu baada ya kuwasili nchini Ijumaa.

Mkurugenzi Mkuu wa DCI, George Kinoti, alikuwa amemlaumu mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati, kwa “kudanganya” kuhusu mahali walikokuwa wakielekea watu hao watatu.

Kwenye taarifa yake awali, Bw Chebukati alidai watu hao ni wafanyakazi wa kampuni ya Smartmatic, ambayo imepewa kandarasi ya kusimamia masuala ya teknolojia na mitambo ya kuendeshea uchaguzi.

Bw Kinoti alisema Bw Chebukati hakueleza ukweli kuhusu ikiwa watu hao walikuwa na mkataba na IEBC au la, pamoja na maelezo yaliyo kwenye mitambo waliyonaswa nayo na polisi.

Bw Chebukati alisema kuwa kinyume na madai ya polisi, raia hao bado wanaendelea kuzuiliwa.

Alisema pia polisi hawajaachilia simu za mikononi, vipakatalishi na mitambo mingine ambayo “ina maelezo muhimu yanayohusiana na uchaguzi wa Agosti 9 na miradi mingine muhimu wanayoendesha katika mataifa mengine”.

Hadi tukienda mitamboni Jumatatu usiku, Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Bw Hussein Marjan hakuwa amejibu maswali aliyotumiwa na Taifa Leo.

Miongoni mwa maswali aliyoulizwa ni kuhusu msimamo wa tume hiyo kuhusu taarifa iliyotolewa na DCI; kuhusu ikiwa raia hao wameachiliwa na polisi au la na hatima ya teknolojia ya kuendesha uchaguzi huo.

Hii ni ikizingatiwa kuwa Bw Chebukati alikuwa amedai kywa teknolojia hiyo imeingiliwa baada ya raia hao kuitishwa maelezo muhimu yanayohusiana nayo. Alikuwa pia amedai polisi wametwaa mitambo muhimu kutoka kwa raia hao.

Tume ilitaka kueleza kuhusu umuhimu wa vibandiko vya kutambua mitambo ya kuendeshea uchaguzi, jinsi itakavyowasilishwa katika maeneo tofauti nchini na jinsi kutwaliwa kwa mitambo hiyo kutakavyoathiri shughuli za matayarisho ya uchaguzi huo, ikizingatiwa zimebaki siku 13 pekee.

Tuliitaka pia tume hiyo kueleza uhusiano wake na Bw Abdullahi Abdi, aliye afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Seamless Technologies, yenye makao yake jijini Nairobi.

Aidha, tuliitaka tume hiyo kueleza ikiwa ilikuwa na mkataba wowote wa utendakazi na kampuni hiyo au kampuni ya Smartmatic kuhusu utoaji wa huduma za kiteknolojia kwenye uchaguzi huo mkuu.

Kulingana na Bw Kinoti, uwepo wa vibandiko vya kutambua mitambo ya KIEMS kwenye mzigo wa raia hao watatu, ni hatari.

Mitambo hiyo ndiyo itakayotumiwa kuwatambua wapigakura na kutuma matokeo kwenye uchaguzi huo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii