Kuna sintofahamu imeibuka kuhusu sarafu ya Sh500 baada ya kuonekana baadhi zenye alama tofauti kwenye mzunguko ambao unaonesha
kuwa sarafu hizo zenye baadhi ya alama tofauti zipo kwenye mzunguko na zinatumika kufanya manunuzi mbalimbali hususan jijini Dar es Salaam.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilipoulizwa imesema inaendelea na uchunguzi wa suala hilo.
Kwa mujibu wa Sheria ya BOT ya mwaka 2006, mamlaka pekee ya kutengeneza, kutoa fedha, kubuni na kuagiza (noti na sarafu) kwa uhalali wa malipo na kukidhi mahitaji.
Julai 11, mwaka huu maofisa wa BoT waliokuwa kwenye maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam walipoulizwa na kuonyeshwa moja ya sarafu hizo, walimtaka mwandishi wa gazeti awasiliane na wizara kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, alipoulizwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alishauri suala hilo lipelekwe Idara ya Sarafu ya BoT huku akitoa onyo vya vitendo vyovyote vinavyohusiana na kuchapisha na kusambaza noti au sarafu.
Idara ya fedha ya BoT ililitaka gazeti hili liandike barua kwa Ofisi ya Gavana wa BoT kuomba ufafanuzi kupitia watalaamu wa idara hiyo.
Baada ya kuandika barua hiyo Julai 14 na Gavana wa Benki Kuu, Profesa Florens Luoga amethibitisha kuipokea na kuwa tayari wameanza uchunguzi.
“Tumepokea barua yenu, suala hili tunalifanyia kazi,” alijibu Profesa Luoga Julai 21.