KITUO cha utafiti na ubunifu kimezinduliwa katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya ili kuwaongeza maarifa wanafunzi wa chuo hicho.
Naibu Chansela wa chuo hicho Prof Deogratius Jaganyi alisema utafiti na ubunifu uliofanywa na wanafunzi hapo awali imeleta matokeo mema yanayonufaisha wengi.
Alisema chumi zinazondelea na zilizoendelea husababishwa na maswala ya ubunifu.
“Baadhi ya nchi zinazoendelea zinazingatia sana maswala ya utafiti na ubunifu ili kufikia mahali zilipo,” akafafanua Prof Jaganyi.
Alieleza kuwa ubunifu na utafiti kwa pamoja hustawisha mataifa kama China, India, na hata Korea. Alisema mataifa hayo yalizingatia utafiti na ubunifu kabla ya kufika mahali yalipo kiuchumi.
Kituo cha utafiti kilizinduliwa siku chache zilizopita MKU mjini Thika na afisa mkurugenzi mkuu wa hazina ya Enterprise Development Fund, Bw Benson Muthendi.
Bw Muthendi alisema uchumi wa nchi umeboreshwa kutokana na ubunifu na ushindani wa kiuchumi na kiteknolojia unaozingatiwa katika maendeleo.
Kituo hicho kipya kilisajili wanafunzi 20 ambao watajitosa ulingoni ili kuingilia maswala ya utafiti mwaka huu wa 2022.
Kituo hicho pia kitapokea ufadhili wa Sh2 milioni kwa wale wote wanaohusika kwenye mradi huo.
Baadhi ya vitu muhimu vilivyoko katika kituo hicho ni vifaa vya kisasa vya hali ya juu na wataalamu waliohitimu watakaojitolea kufanikisha ubunifu na utafiti wa aina yoyote.
Bw Muthendi alisifu kituo hicho kama eneo la kukuza vipaji vya vijana ambao watapokea ujuzi utakaowapa ajira hapo baadaye.
Wakati wa kuonyesha ujuzi wa kiutafiti Githinji Gatambu, aliibuka mshindi miongoni mwa watu 20 walioteuluwa kushiriki.
Utafiti wake ulihusu mabaki ya taka za plastiki katika mitaa ya makazi.
Wa pili katika utafiti huo alikuwa Nthuku Mumo, huku Margaret Wambui Wahome akikamata nafasi ya tatu.
Mwekezaji wa kibiashara, Dkt Josephat Karanja, aliwashauri vijana ambao wanaendesha utafiti wa aina tofauti kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu ili waweze kufanikiwa.
Mwanzilishi wa chuo hicho Prof Simon Gicharu alisema utafiti na ubunifu ni mambo mawili muhimu yanayostahili kuzingatiwa kwa undani hasa na wanafunzi.
Alisema kutokana na hali hiyo maswala hayo yana mabadiliko makubwa katika mashirika makubwa na hata maisha ya binadamu.
“MKU ni kitengo muhimu cha kufanyia utafiti na tunawapa nafasi wanafunzi kuonyesha ujuzi wao. Tunazingatia utu na maswala ya utafiti,” alifafanua Prof Gicharu.
Alisema ili kupambana na maswala ya ukosefu wa kazi barani Afrika, ni vyema kuwa na wanafunzi wengi walio na ujuzi ambao ni wabunifu katika maswala tofauti.
“Ninawahimiza vijana kuwa na moyo wa kujituma wenyewe bila kushurutishwa kutenda jambo huku wakishauriwa kuzuru kituo hicho kila mara ili kujifunza mengi,” alifafanua Prof Gicharu.
Naye Pro-Chansela wa chuo cha Mount Kenya Dkt Vincent Gaitho, alisema kuzinduliwa kwa kituo hicho ni hatua muhimu kwa wanafunzi kwa sababu inawapa mwelekeo mwema wa kimaisha.
Alisifu sana sekta ya binafsi – KEPSA – kwa kuunga serikali mkono kuhusiana na maswala ya ajira.
Alisema wanafunzi wana nafasi njema ya kujiongeza maarifa zaidi kwa kuzingatia maswala ya utafiti na ubunifu.