Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza Liz Truss amethibitisha nia yake ya kugombea nafasi ya Waziri Mkuu wa Nchi hiyo iliyo wazi baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Nchi hiyo Boris Johnson kujiuzulu wiki iliyopita.
Truss ambaye pia ni mbunge kutoka Chama Tawala cha Conservative amesema uzoefu alionao katika medani za uhusiano wa kimataifa ikiwemo mchango wake katika kuiwekea vikwazo nchi ya Urusi kufuatia uvamizi ndani ya Taifa la Ukraine vinampatia ujasiri wa kuona yeye ni mtu sahihi wa kuziba nafasi hiyo na kuifikisha Uingereza pale inapotarajia kufika.
“Najitokeza mbele kwa sababu naamini naweza kuongoza, kufanikisha lakini pia kutekeleza maamuzi magumu. Ninao mtazamo chanya wa hasa wapi tunatakiwa kufika na uzoefu wa kuhakikisha tunafika hapo. Alisema Liz.
Truss ni sehemu tu ya wanasiasa wengi waliojitokeza kuwania nafasi hiyo akiwemo Kansea Nadhim Zahawi, Katibu Mkuu wa Usafirishaji Grant Shapps, Kansela wa zamani Rishi Sunak, Mwanasheria Mkuu Suella Braverman pamoja na Waziri wa Zamani wa Haki na Usawa Jeremy Hunt.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Shirika la Utangazaji la CNN ni kwamba wagombea wote watapitia hatua mbalimbali za mchujo ndani ya Chama Tawala cha Conservative hadi pale watakaposalia wagombea wawili tu.