MNAMO Jumamosi iliyopita, viongozi wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) walitangaza kuiondolea vikwazo Mali, kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika nchini humo Mei 2021.
Kwenye tangazo hilo, ECOWAS ilisema ilikubali kuiondolea Mali vikwazo hivyo baada ya viongozi wake wa kijeshi kukubali kurejesha uongozi wa taifa hilo ndani ya muda wa miaka miwili.
Tangazo hilo ni afueni kubwa ya kisiasa na kiuchumi kwa Mali, ikizingatiwa karibu mataifa hayo yote yalikuwa yamefunga mipaka yake, hivyo kuifanya nchi hiyo kama kisiwa kidogo kilichozungukwa na bahari kubwa yenye dhoruba hatari.
Bila shaka, Mali si taifa la kwanza katika eneo hilo na kwingineko barani Afrika kukumbwa na mapinduzi ya kijeshi au vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kando na Mali, nchi zingine ambazo zimeathiriwa na mapinduzi ya kijeshi ni Burkina Faso, Nigeria, Gambia kati ya mengine.
Baadhi ya yale yanayokumbwa na ghasia ni DRC Congo, Chad, Ethiopia, Somalia, Sudan, Sudan Kusini kati ya mengine.
Tathmini hiyo inaashiria kuwa Waafrika bado wanaendelea kuzozana baada ya nusu karne tangu kujinyakulia uhuru.
Hata hivyo, kuna pendekezo la awali, ambalo lishawahi kutolewa na viongozi kadhaa, kuhusu Afrika kuungana na kubuni nchi kubwa, kama vile Amerika, Urusi au Jumuiya ya Ulaya (EU).
Pendekezo hilo lilitolewa na aliyekuwa kiongozi wa Libya kwa muda mrefu, Muammar Gaddafi.
Kabla ya mauaji yake 2011, Gaddafi alishikilia uwepo wa miungano kama vile Umoja wa Afrika (AU) haukuwa ukiisaidia Afrika kutatua changamoto za kisiasa, kijamii na kiuchumi zilizokuwa zikiyaandama mataifa mengi.
Alitoa mfano wa Amerika, aliyosema kuwa moja ya sababu zilizoyawezesha majimbo ya Kusini na Kaskazini kuungana na kubuni nchi moja ni uwepo wa sarafu moja, serikali moja na mfumo wa utawala unaokubalika na kuheshimika na kila jimbo.
Ingawa kufikia wakati wa kifo chake mataifa ya Ulaya hayakuwa yamebuni na kukubaliana kutumia sarafu ya Euro, Gaddafi alisifia sana hatua za mwanzo zilizokuwa zikipigwa na EU.
Vivyo hivyo, ikizingatiwa AU inatimiza miaka 50 mwaka ujao tangu kuanzishwa kwake 1963, huu ndio wakati mwafaka kwa Afrika kutathmini na kukumbatia pendekezo la Gaddafi, kwani changamoto zilizoikumba katika miaka ya sitini bado zingalipo.
Labda kwa kuiiga Amerika, Ulaya na Urusi, huo utakuwa mwanzo wa Afrika kupata suluhisho kwa changamoto zake.