NI kawaida kutembea bila viatu kwenye fuo za bahari katika visiwa vingi ulimwenguni.
Lakini katika Kaunti ya Lamu, ni kawaida kukumbana na wanaume wakitembea bila viatu hadi katikati ya mji na vichochoroni.
La kushangaza ni kuwa, ni kawaida kwao kuingia hata kwenye ofisi za serikali wakiwa hajavalia chochote mguuni mwake.
Baadhi ya wageni huwachukulia kuwa wasio na ustarabu watu hao ni mwehu au mshamba, wakishangaa ni kwa nini wanashindana na kuku wanapotembea. Lakini, kuna wale wageni ambao huvutiwa na hulka hii ya kipekee kiasi cha kuwaiga wenyeji.
Bakari Muhaj, 56, ambaye ni mvuvi, asema kazi yake imemsukuma kuepuka kabisa viatu, iwe ni champali au buti kwenye miguu yake.
Bw Muhaj asema karibu asilimia tisini ya maisha yake huwa hana viatu.
“Utavaaje viatu ukiwa ukitarajia kuingia baharini kuvua samaki? Mimi hupendelea kwenda baharini miguu chuma na nikitoka, hutembea tu nyayo kavu bila viatu. Muda ninaopata kuvaa champali ni ule wa kwenda msalani nikiwa ndani ya nyumba,” asema Bw Muhaj.
Bw Ali Swaleh, 55, anasema katika ujana wake alizoea kuona wazee wakitembea bila viatu, hivyo pia akaamua kuishi akipiga guu kwa lami.
Bw Swaleh anasema kila anapovaa viatu humtatiza kutembea kwa kasi.
“Nilimshuhudia babangu akiwa havai viatu, iwe anaenda safari au shughuli zake za kila siku ambazo ni uvuvi. Mimi pia sikuona haja ya kujitatiza kuvaa viatu. Ni mwaka wa 30 sasa tangu nikome kuingiza kiatu kwenye mguu wangu na ninahisi furaha zaidi nikitembea nyayo tupu,” akasema Bw Swaleh.
Bw Amin Miji ambaye ni mhudumu wa kutembeza watalii ufuoni asema ni vigumu kwao kuvaa viatu kwenye mazingira ya ufuoni kutokana na mchanga mwingi unaopatikana maeneo hayo.
Kwa upande wake, Bw Abdullahi Islam anasema hajawahi kuvalia viatu tangu kuzaliwa kwake kutokana na joto jingi Lamu.
Tabia hiyo ya wanaume wa Lamu kutembea bila viatu pia imeanza kuenziwa na wageni, ikiwemo watalii wa ndani kwa ndani na pia wale wa ng’ambo.
“Mimi nikifika Lamu, huweka kando viatu na kutembea mguu chuma hadi wakati likizo yangu imekamilika na ninastahili kuabiri ndege kurudi Uingereza,” akasema mtalii, Bw Nathan Theo.
Wataalamu wa Afya walisema kutembea bila viatu kuna manufaa tele kiafya ikiwa mazingira ni masafi.
Dkt Duncan Chai wa Kituo cha Afya cha Blueline Mkoroshoni, Kaunti ya Kilifi alisema hatua hiyo huzidisha nguvu za viungo na pia kuiweka akili katika hali nzuri na hata kupata usingizi bora usiku.
Naye daktari mkuu wa Kaunti ya Lamu, Chris Margan, alihimiza wananchi wengine kuiga mfano huo kwani huenda ikampunguzia mhusika maumivu ya viungo.
“Mara nyingi unapovaa viatu unapata hata kusimama ni shida. Ukitembea mguu chuma nakuhakikishia hutahisi maumivu kama hayo,” akasema Bw Margan.