Katibu Mkuu wa OPEC Barkindo afariki ghafla akiwa na umri wa miaka 63

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani - OPEC, raia wa Nigeria Mohammed Barkindo, amefariki dunia ghafla akiwa na umri wa miaka 63. Kifo hicho kimetangazwa na afisa mkuu mtendaji wa Shirika la Mafuta la Nigeria - NPC Mele Kyari, ambaye amesema Barkindo alifariki dunia saa tano jana usiku. Hakutoa maelezo kuhusu mazingira ya kifo chake. Barkindo alikuwa nyumbani Nigeria kwa ajili ya mkutano wa kilele wa nishati mjini Abuja, na alikuwa amezungumza na Rais Muhammadu Buhari hapo jana. Wakati wa mkutano huo alitoa hotuba inayoonya kuwa sekta ya mafuta na gesi ulimwenguni iko hatarini. Alitarajiwa kukabidhi wadhifa huo kwa Haitham Al Ghais wa Kuwait Agosti mwaka huu. Tangu alipochokua usukani wa OPEC mwaka wa 2016, Barkindo aliongoza katika nyakati ngumu kwa muungano huo wa wazalishaji mafuta, ambazo zilishuhudia masoko yakiyumba kutokana na matukio ya kihistoria kama vile COVID-19, kutengenezwa kwa muungano wa OPEC+ na Urusi na mataifa mengine yasiyo ya OPEC, na uvamizi wa Moscow nchini Ukraine.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii