VIJANA waliandama mjini Kisii jana dhidi ya maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) mjini Kisii.
Vijana hao walikabiliana na maafisa wa polisi katika kituo cha Itumbe na kulemaza usafiri katika barabara kuu ya Kisii- Kilgoris.
Fujo zilianza vijana hao walipojaribu kuvamia afisi za IEBC za Bobasi kwa lengo la kuwatimua maafisa waliokuwa ndani.
Jengo hilo ambalo lina afisi za IEBC, linasimamiwa kwa karibu na maafisa wa polisi kwani pia linatumika kama makao makuu ya Kaunti Ndogo ya Sameta.
Kufuatia hali hiyo, maafisa wa polisi waliwarushia vitoa machozi vijana hao wasiotii, na wakatawanyika kukimbilia usalama wao.
Wengi wa waandamanaji hao walikuwa na nyuso zinazofahamika za waendeshaji bodaboda katika mji wa Kisii.
Waandamanaji hao baadaye walijipanga upya na kuziba barabara kuu ya Kisii-Kilgoris huku wakiwasha moto kwa kuyachoma magurudumu chakavu ya magari.
Takriban vijana watano walikamatwa kuhusiana na maandamano hayo.