Matajiri wa Chamazi raundi hii hawataki utani kabisa na bosi mkubwa, Yusuf Bakhresa ameingilia usajili na hadi sasa ameshusha wageni watano wa maana na wazawa watatu hatari.
Isah Ndala kutoka Plateau ya Nigeria, Tape Edinho na Kipre Junior wote wa Ivory Coast, Ahmada kutoka Comoro na Mghana James Akaminko kutoka Great Olympic ni wageni walioshushwa hadi sasa huku wazawa wakiwa Nathanael Chilambo kutokea Ruvu Shooting, Cleophace Mkandala kutoka Dodoma Jiji na Sopu kutoka Coastal Union na sasa ipo mbioni kukamilisha usajili wa mwisho kwa kushusha beki hatari.
Mastaa hao wakiungana na wale waliokuwepo msimu uliopita, chama hilo chini ya Kocha Abdihimid Moallin litabadilika na huenda likawa hivi;
Ahmada ndiye atasimama langoni na beki ya kulia atamaliza Chilambo wakati kushoto akicheza Kangwa na kati watasimama Daniel Amoah na Aggrey Morris, japo bado wanasikiliza beki mwingine mkali zaidi wa kimataifa kufungia usajili wao.
Viungo wawili wa chini watacheza Ndala na Akaminko huku juu yake wakitawala mafundi watatu, Sopu, Kipre na Edinho na pale mbele atamaliza Rogers Kola.
Benchi hapo unawakuta kina Wilbol Maseke, Abdalah Sebo, Sospeter Bajana, Keneth Muguna, Idris Mbombo, Iddi Nado na Prince Dube.