RAIS Uhuru Kenyatta ametumia Sh1.5 trilioni kwa ujenzi wa barabara katika kipindi cha zaidi ya miaka tisa ya utawala wale, na ataondoka Agosti akiwa amewaachia Wakenya kilomita 11,000 za barabara ya lami.
Uchunguzi kuhusu utumizi wa pesa katika ujenzi wa barabara unaonyesha kuwa utawala wa Jubilee ulitumia jumla ya Sh1.44 trilioni kujenga barabara kati ya Juni 2013 na Machi 2022.
Takwimu kutoka kwa Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) zinaonyesha kuwa matumizi ya pesa kwa ujenzi wa barabara yalipanda kutoka Sh87.6 bilioni mwaka wa kwanza alipoingia ofisini, hadi Sh207 bilioni kwa mwaka, mwaka 2021.
Matumizi ya juu zaidi kwenye mpango huo yalikuwa kwenye awamu ya pili ya uongozi wake, (2017-2022), ambapo serikali ilitumia Sh951 bilioni, ikilinganishwa na ilivyotumia Sh490 bilioni katika awamu yake ya kwanza.
Kwenye hutoba yake ya mwisho kama rais wakati wa sherehe za madaraka Dei, Rais Kenyatta alijigamba kwamba chini ya uongozi wake, serikali imetengeza barabara nyingi zaidi ikilinganishwa na tawala zote zilizotangulia.