"Afghanistan ya leo ni tishio kubwa zaidi kwa usalama wa dunia kuliko ilivyokuwa mwaka 2001." Hili ni onyo kali kutoka kwa mtoto wa kiongozi maarufu wa upinzani dhidi ya Taliban.
Ahmad Massoud ana umri wa miaka 33 tu lakini tayari anafuata nyayo za babake. Baba yake alikuwa kamanda mwandamizi Ahmad Shah Massoud, anayejulikana kama 'simba wa Panjshir', jimbo la kaskazini mwa Kabul ambako familia hiyo inatoka. Aliuawa na maafisa wa al-Qaeda siku mbili kabla ya mashambulizi yao ya 9/11 dhidi ya Marekani mwaka 2001.
Hii ilikuwa katika kipindi cha mwisho cha utawala wa Taliban wakati kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Afghanistan liliruhusu makundi mengine ya kijihadi kuishi katika ardhi yake.
Sasa, mtoto huyo anaogopa namna historia inavyojirudia.
'Mahali salama zaidi kwa magaidi'
Ahmad Massoud anasema nchi yake kwa mara nyingine imekuwa kimbilio salama kwa makumi ya makundi ya kigaidi, yakiwemo ISIS na al-Qaeda, yanayotaka kusambaza itikadi zao kali kila mahali duniani. Serikali ya Afghanistan inayoungwa mkono na nchi za Magharibi ilianguka mwezi Agosti mwaka jana kufuatia kuondolewa kwa wanajeshi wa kigeni.
Kundi la Taliban lilichukua tena madaraka baada ya zaidi ya miaka 20 ya kupambana na uasi dhidi yao., Ahmad Massoud anaonya ulimwengu dhidi ya kupuuza Afghanistan, akisema nchi yake inahitaji uangalizi wa haraka na utulivu wa kisiasa.
Anasema makundi ya kigaidi yangetumia msukosuko huo kujaribu kushambulia maslahi ya kigeni.
Baba yake marehemu, Ahmad Shah Massoud, alitoa onyo kama hilo siku chache kabla ya 9/11. Ahmad Massoud anasema onyo la baba yake halikuzingatiwa na dunia imeishi na matokeo yake tangu wakati huo. Bwana Massoud anaelezea hali ya Afghanistan kuwa mbaya zaidi kuliko wakati wa baba yake.
"Ninatumai dunia na hasa Ulaya inaelewa ukali wa vitisho kutoka Afghanistan na kuingilia kati kwa njia ya maana kusaidia kuanzisha serikali inayowajibika na halali nchini Afghanistan," alisema.