Saudi Arabia imesema itafungua anga yake kwa mashirika yote ya ndege, hatua hiyo ikitoa fursa kufanyika kwa safari za ndege za kutoka na kuelekea Israel. Uamuzi huo umekaribishwa na rais wa Marekani Joe Biden ambaye anatarajiwa kufanya ziara leo Ijumaa katika nchi hiyo ya utawala wa kifalme. Mamlaka ya usafiri wa anga ya Saudi Arabia- GACA imesema anga ya nchi hiyo sasa iko wazi kwa mashirika yote ya ndege ilimradi tu ndege hizo zitatimiza masharti yake ya usafiri, kulingana na mikataba ya kimataifa inayoeleza kuwa hakupaswi kuwa na ubaguzi juu ya safari za ndege za abiria. Katika taarifa, mamlaka hiyo imeongeza kuwa uamuzi huo utaimarisha juhudi za kuifanya Saudia kama kitovu cha kimataifa cha kuunganisha mabara matatu. Rais Joe Biden ameupongeza uamuzi huo kwa kusema ni hatua muhimu kuelekea kupata uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati.