Klabu ya Simba juzi ilimtambulisha kocha mkuu, Zoran Maki ambaye
ameelewa matumaini mapya ndani ya klabu hiyo msimu ujao na akiwataka
wapinzani wake wajipange kwani yuko tayari kwa kazi.
Zoran ambaye
amesaini mkataba wa mwaka mmoja akichukuwa nafasi ya Mhispania Pablo
Franco, ametamba kwamba kipaumbele chake ni kufanya kitu cha tofauti na
Simba msimu ujao na kuivusha kwenye hali iliyopo sasa.
Amesisitiza
kwamba anataka kufanya makubwa zaidi ya alivyofanya kwenye Ligi za
Sudan, Morocco na Algeria ambako ni kugumu kama Tanzania lakini ametamba
pia haihofii dabi ya Agosti 13 dhidi ya Yanga kwavile amezoea mechi
kama hizo na atakuwa na wachezaji wazuri na atakaowapa malengo.
Akizungumza
wakati wa utambulisho wake, Zoran alisema; "Nilicheza mechi 15 ndani ya
miezi miwili na isitoshe ningekuwa Ulaya ningepewa miaka minne ila huku
ni tofauti hivyo nina uzoefu na soka la Afrika na hakuna shida juu ya
hilo kwani jambo kubwa ni ushirikiano."
"Siwezi kutoa ahadi kubwa
kwenye michezo ya kimataifa ingawa ninachotaka ni kufanikisha mambo,
tuwe na mwenendo mzuri kwenye michuano mbalimbali na kurejesha heshima
ya Simba ambayo msimu uliopita ilikosekana," alisema.
"Nataka kufanya
vizuri zaidi ya huku nilikotoka na hili linawezekana kama tukiwa na
ushirikiano mzuri, Simba ni klabu kubwa Afrika hilo
halipingiki,"aliongeza na kusisitiza kwamba anatamani kucheza zaidi ya
nusufainali ya Afrika alikofika na Wydad Casablanca.
Zoran aliongeza
kuwa ligi ya Tanzania ni nzuri na yenye ushindani akiifananisha na ya
Angola kwani asilimia kubwa mabingwa ni wale wale waliozoeleka tofauti
na nchi za Morocco na Algeria ambazo zinaweza kutoa bingwa yoyote.
Kuhusu
mkataba wake, Zoran alisema kupewa mkataba wa mwaka mmoja sio kitu
kibaya kwake kwani sehemu zingine wanatoa mkataba wa miezi sita.
“Nina
uzoefu wa soka la Afrika huwa wanatoa mkataba wa miezi sita, huu wa
mwaka mmoja ni mzuri japokuwa itanichukua hata miezi sita kwanza kujua
namna ambavyo soka la hapa linavyokwenda,” alisema Zoran.
Zorani
alisema anaifahamu Simba baada ya kuiona kwenye mashindano ya CAF na
hata aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Didier Gomes alikuwa anamfuatilia
vizuri.
“Naijua Simba kwa sababu nimeona mechi zao za CAF, Yanga
naijua kidogo sana maana sijawahi kuona mechi zao, Kocha wa zamani
Simba, Didier nilikuwa naye Ligi ya Sudan na nilimfunga ila ni kocha
mzuri sana,” alisema Zoran ambaye amewahi kuzifundisha timu za Wydad Ac
(Morocco), Al Hilal (Sudan) na CR Belouizdad .
Naye Meneja
Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally alisema viongozi wao wote
walijiridhisha juu ya ubora na uzoefu wa kocha huyo hasa soka la Afrika
kitu ambacho ndicho kigezo kikuu kilichozingatiwa katika kumuajiri.
Miongoni
mwa malengo aliyopewa kocha huyo ni kuhakikisha timu inachukua ubingwa
wa Ligi Kuu Bara ambao iliukosa msimu ulioisha, kuchukua Kombe la
Shirikisho la Azam (ASFC) na kuifikisha hatua ya nusu fainali ya Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Baada ya kutua nchini zoran atajiunga na kikosi
hicho kwenye maandalizi ya msimu mpya wakati kitakaposafiri Julai 14
kwenda Misri ili kuweka kambi huku mtihani wake wa kwanza ni dhidi ya
Yanga katika Ngao ya Jamii Agosti 13.
Kuhusu safari yao ya Misri,
Ahmed alisema; “Tunaondoa Julai 14 mwezi huu na tutakuwa hadi Agosti 8
tutarudi kwa ajili ya Simba Day pamoja na mchezo wa kwanza wa ufunguzi
wa Ligi,
“Tutakuwa na wachezaji wote kasoro wale ambao watakuwa
kwenye timu za Taifa ambao tutawaacha wakiwa na majukumu mengine.”
alisema na kuongeza;
“Zoran yupo hapa kuhakikisha Simba inapata
ubingwa wa Ligi, Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho pamoja na kuingia
nusu fainali Caf,” alisema Ahmed.