Ndivyo unavyoweza kumwelezea Rished Bade, ambaye aliwekwa kando kwa miezi 79 tangu alipoondolewa katika wadhifa wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na sasa ameibuka akiwa Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha na Mipango.
Bade ni miongoni mwa viongozi wa mwanzo kutumbuliwa na Dk John Magufuli, Rais wa awamu ya tano ikiwa ni takribani siku 20 tangu mkuu huyo wa nchi aapishwe kuwa Rais Novemba 5, 2015.
Kutumbuliwa kwa Bade kulitokana na kile taarifa ya Ikulu ilichokieleza kuwa, akiwa kamishna mkuu wa TRA mamlaka hiyo iliisababishia Serikali hasara ya Sh80 bilioni kwa kushindwa kutoza ushuru makontena 349 yaliyoingia nchini.
Msomi huyo wa usimamizi wa biashara alitumbuliwa baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam na kubaini kasoro hizo.
Hivi karibuni, picha ilionekana mitandaoni ikimwonyesha Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akisalimiana na Bade, aliyetambulishwa kwa cheo cha Kamishna wa Fedha za Nje wa wizara hiyo.
Aidha, Bade alikuwa miongoni mwa maofisa waliohudhuria mazungumzo baina ya Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia kanda ya mashariki, Victoria Kwakwa, yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Vilevile, tovuti ya wizara hiyo imemtaja Bade kama Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango, wadhifa ambao ameupata baada ya Sauda Msemo aliyekuwa akishika nafasi hiyo kuteuliwa na Rais Samia kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
Sauda aliteuliwa Mei 25 mwaka huu akichukua nafasi ya Dk Bernard Yohana Kibesse, ambaye aliteuliwa kuwa Balozi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande kutaka kujua Bade alianza lini kushika wadhifa huo ambapo alisema ni wiki chache tangu kiongozi huyo atwae wadhifa huo.
Alisema nafasi hiyo huteuliwa na Waziri wa Fedha na Mipango kwa baraka za rais.
“Waziri ndiyo anawateua makamishna lakini baada ya baraka za Rais. Hata juzi tulipokwenda Ikulu Rais alimuita kamishna mpya,” alisema Chande.
Bade alihudumu TRA tangu mwaka 2012 kwa nafasi ya naibu Kamishna wa mamlaka hiyo hadi Mei 6, 2014 alipoteuliwa na Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete kuwa kamishna mkuu.
Uteuzi wake ulitokana na kustaafu kwa aliyekuwa na wadhifa huo, Harry Kitilya.
Kabla ya utumishi wake katika mamlaka hiyo ya Serikali, kwa sehemu kubwa Bade ametumikia katika taasisi za benki akianzia nafasi ya ukaguzi wa Benki za biashara, Benki Kuu ya Tanzania mwaka 1995 hadi mwaka 2000.
Baadaye mwaka 2000-2001 alihamia benki ya Akiba kwa nafasi ya meneja mikopo, kisha akahamishiwa nafasi ya ofisa fedha mkuu.
Mwaka 2006 alitumikia nafasi ya mwendeshaji mkuu wa benki ya Barclays nchini Uganda na baadaye mwaka 2007 hadi 2009 alikuwa mtendaji mkuu wa benki hiyo kwa upande wa Tanzania.
2009-2012 alikuwa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo kwa upande wa Afrika mashariki na magharibi na mwaka 2010-2012 alikuwa mtendaji mkuu wa Tanzania Mortgage Refinance Company.