Wanaharakati wa kupambana na mihadarati eneo la Pwani wamepinga vikali sera za baadhi ya wagombea urais, zinazolenga kuhalalisha matumizi ya bangi iwapo wataingia madarakani.
Wakiongozwa na Mohammed Famau wanaharakati hao walisema sera hizo ni pigo kwa vita dhidi ya ulanguzi wa mihadarati nchini.
Akizungumza mjini Malindi katika Kaunti ya Kilifi, Bw Famau aliwataka wanasiasa hao kujiepusha na siasa ambazo zitapotosha jamii kimaadili.
“Kuna baadhi ya viongozi wamejitolea wazi kwamba ikiwa watachaguliwa watahalalisha matumizi ya bangi na kuifanya kuwa biashara kuu. Hii itafanya vijana wajue bangi ni halali badala ya kujiepusha nayo. Viongozi wajiepushe na matamshi ya kuwafanya vijana waingilie dawa za kulevya,” alisema Bw Famau.
Meneja wa masuala ya maendeleo katika shirika la KECOSCE Kaunti ya Kilifi, Bw Joseph Siyanda, alilitaja pendekezo hilo kama propaganda za wanasiasa kujitafutia umaarufu miongoni mwa wapigakura.
“Hauwezi kuwa na sera nzuri kwa wananchi ikiwa unawaambia watu watumie mihadarati,” alisisitiza Bw Siyanda.
Aidha Siyanda amewataka wanasiasa wote humu nchini kufanya kampeni zilizo na maadili na sio za kupotosha taifa hili.
Hata hivyo, idadi kubwa ya vijana katika eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi wanadaiwa kutokuwa na maadili mema katika jamii.