Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa leo limetoa wito wa kufanyika mageuzi kwenye mifumo ya afya ya akili duniani likisema kuna ongezeko la matatizo ya akili tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona.Katika hafla ya uzinduzi wa tathmini pana ya afya ya akili ambayo ni kubwa kuwahi kufanywa na WHO tangu kuanza kwa karne ya 21, shirika hilo limesema hali ya msongo wa mawazo na sonona duniani imepanda kwa asilimia 25 katika mwaka wa kwanza wa janga la corona.Mnamo mwaka 2019 kabla ya kuzuka kwa janga hilo WHO ilikadiria watu bilioni moja walikuwa wanaishi na matatizo ya akili.Miongoni mwa mambo yanayochangia msongo wa mawazo ni udhalilishaji wa kingono na uonevu wakati wa utoto. WHO imeyarai mataifa kuchukua hatua kushughulikia suala la matatizo ya akili kwa kubuni mipango itakayowasaidia wenye uhitaji.