RAIS UHURU KENYATTA AWAKERA MAAFISA WA SOMALIA

RAIS Uhuru Kenyatta alijipata pabaya baada ya kualika maafisa wa jimbo la Somaliland katika dhifa iliyohudhuriwa na balozi wa Somalia, Jumanne jioni.

Katika dhifa hiyo kulikuwa na bendera ya Somaliland ambayo imejitangaza kuwa nchi huru – japo haitambuliwi na Umoja wa Mataifa.

Somaliland ilijitangaza kuwa nchi huru miaka 30 iliyopita lakini Somalia inaichukulia kama moja ya majimbo yake.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Kenya ililazimika kuomba msamaha Balozi wa Somalia humu nchini huku ikisema ‘lilikuwa kosa kubwa’ kujumuisha bendera ya Somaliland katika dhifa hiyo iliyofanyika katika Ikulu ya Nairobi.

“Wizara inaomba radhi na Kenya inatambua kuwa kuna serikali moja tu ya Somalia,” ikasema barua iliyotumwa katika ubalozi wa Somalia humu nchini.

Hali ya taharuki ilizuka baada ya balozi wa Somalia humu nchini Mohamoud Ahmed Nur ‘Tarzan’ kusimama ghafla na kuondoka baada ya kuona bendera ya Somaliland ukumbini.

Kutia msumari kwenye kidonda, mwakilishi wa serikali ya Somaliland pia alikuwepo.

Somaliland ina ofisi yake jijini Nairobi lakini Somalia haijapinga.

Somalia pia imewahi kuruhusu Kenya kuweka afisi za ubalozi mdogo katika mji wa Hargeisa, ambao ni makao makuu ya Somaliland.

Nur alisema kuwa aliamua kususia hafla ya Rais Kenyatta baada ya kubaini kuwa mwakilishi wa Somaliland alikuwa amepewa hadhi sawa na mabalozi.

Uhasama huo ulitokea siku chache baada ya Rais Kenyatta na mwenzake wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud kuafikiana kurejesha uhusiano mwema baina ya mataifa hayo jirani.

Kenya imekuwa ikihimiza Somalia na Somaliland kufanya mazungumzo ili kutatua mvutano uliopo.

Wakati wa utawala wa kikoloni, Somaliland ilikuwa ikitawaliwa na Waingereza huku Somalia ikitawaliwa na Waitaliano.

Mnamo 1960 maeneo hayo mawili yaliungana na kuunda Jamhuri ya Somalia.

Mnamo 1991 Somaliland ilitangaza kujitenga.

Kuanzia wakati huo Somaliland imekuwa ikiendesha jeshi lake, serikali, benki kuu na sarafu yake.

Taiwan – ambayo inatambuliwa kimataifa kuwa sehemu ya China – inatambua Somaliland kama nchi huru.

Mnamo 2020, Somalia ilikatiza uhusiano wake wa kidiplomasia na Kenya kupinga hatua ya Rais Kenyatta kukutana na kiongozi wa Somaliland Muse Bihi.

Kiongozi huyo wa Somaliland alipozuru Kenya, aliafikiana na Rais Kenyatta kuruhusu safari za ndege za moja kwa moja kati ya Nairobi na Hargeisa.

Lakini Somalia haikuelezea kutamaushwa kwake Rais Bihi alipozuru mataifa ya Djibouti na Ethiopia.

Uingereza, Djibouti na Ethiopia ni miongoni mwa nchi zilizo na balozi mjini Hargeisa.

Mapema mwaka huu wa 2022, Bunge la Uingereza lilijadili hoja ya kutaka kutambua rasmi Somaliland kuwa nchi huru.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii