Straika wa mabao atua Simba

Yanga inafanya  usajili wa bandika bandua kutokana na namna wanavyofanya usajili wao kuelekea msimu wa 2022/23, lakini kama unadhani Simba wamepoa unajidanganya.

Unataka kufahamu kwa upande wa mabingwa watetezi mpango wao upoje? Iko hivi, Simba ambao wanapambana kusaka kocha mpya kwa ajili ya kuziba pengo la Pablo Franco wanafanya usajili wao kimyakimya na tayari straika wa mabao wa Geita Gold, George Mpole amemwaga wino Msimbazi.

Simba ambao wameshindwa kutetea mataji yao mawili la Ligi Kuu ambalo pamoja na kubakiza mechi tano huku vinara wa ligi Yanga wakiwa na mechi nne wanahitaji pointi tatu tu kutawazwa mabingwa wapya na lile Shirikisho la Azam ambalo wameshindwa kutinga fainali, wamemnasa mchezaji huyo ‘kimafia’.

Chanzo cha kuaminika kimeliambia gazeti hili kuwa Simba wanaendelea na mawindo ya kusaka mastaa wengine watakaowarudisha kwenye ushindani msimu ujao na tayari Mpole aliyefunga bao lake la 15 msimu huu dhidi ya Dodoma Jiji, jana wameshamnasa ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu. Geita ilishinda mabao 2-0.

Simba tayari wamefanya mazungumzo na mchezaji huyo ambaye pia amekuwa akipigiwa mahesabu na Yanga kwa ajili ya kuongeza nguvu kikosini mwao natayari ameshafanya mawasiliano na timu zote mbili.

“Mpole alipokuwa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ mara baada ya mchezo wake wa mwisho dhidi ya Algeria ambao Tanzania ilikubali kichapo cha mabao 2-0 mchezaji huyo alibebwa moja kwa moja na kupelekwa moja ya hotel iliyopo katikati ya mji (Dar) ili kufanya naye mazungumzo,” kilisema chanzo hicho. “Mchezaji huyo kakaa kwenye hoteli siku tatu malipo yakiwa chini ya Simba kwa ajili ya mazungumzo hadi anaondoka kuuwahi mchezo na Dodoma Jiji leo (jana) huku mazungumzo yakiwa ni asilimia 80 mchezaji huyo kamalizana na timu hiyo.”


Awali, Mpole alihusishwa kuongeza mkataba wa mwaka mmoja na Geita Gold ambao haumfungi kuondoka, lakini chanzo hicho kimekanusha ishu hiyo na kuweka wazi kuwa mshambuliaji huyo aliigomea ofa ya Geita kutokana na ofa za timu hizo mbili za mitaa ya Kariakoo.

“Mpole mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, hana mkataba na timu yake kwa sababu aligomea ofa baada ya kupata ofa nono kutoka Simba na Yanga,” kilisema chanzo hicho ambacho kililithibitishia gazeti hili kuwa Simba ameipa nafasi kubwa kumsajili kuliko Yanga.

Mwenyekiti wa timu ya Geita gold Constantine Moland aliliambia kuwa wamefanya mazungumzo na Mpole na kumuongeza mkataba wa mwaka mmoja ambao una kipengele cha kuondoka endapo atapata timu nyingine.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii