Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema hadi kufikia
Aprili 2022, deni la Serikali lilikuwa Sh69.44 trilioni ikilinganishwa
na Sh60.72 trilioni kwa kipindi kama hicho mwaka 2021, sawa na ongezeko
la asilimia 14.4.
Kati ya kiasi hicho, deni la nje lilikuwa Sh47.07 trilioni na deni la ndani lilikuwa Sh22.37 trilioni
Dk
Nchemba amesema hayo leo Jumanne Juni 14, 2022 wakati akiwasilisha hali
ya uchumi wa Taifa na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha
2022/23.
Amesema ongezeko la deni la Serikali lilitokana na
kupokelewa kwa mikopo mipya kutoka vyanzo vyenye masharti nafuu na ya
kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Aidha,
ongezeko la deni lilitokana na kutolewa kwa hatifungani maalumu yenye
thamani ya Sh2.18 trilioni kwa ajili ya deni la Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) lililotokana na michango ya
watumishi wa kabla ya mwaka 1999.
Amesema taarifa ya tathmini ya
uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba 2021 inaonesha kuwa deni la
Serikali bado ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na
mrefu kwa kuzingatia ukomo wa viashiria vyote vinavyokubalika kimataifa.