Mashindano yajayo ya kuwania ubingwa wa Afrika AFCON yatafanyika mapema mwaka 2024 ili kuzuia kinyang'anyiro hicho kukumbwa na mafuriko wakati wa msimu wa mvua nchini Ivory Coast ambao kawaida huwa katikati ya mwaka. Kamati ya utendaji ya Shirikisho la Kandanda Barani Afrika CAF imeamua kuahirisha mashindano hayo ambayo yalikuwa yachezwe kati ya mwezi Juni na Julai ila sasa yatachezwa kati ya Januari na Februari. Haya yatakuwa mashindano ya pili mfululizo ya AFCON kufanyika mwezi Januari na Februari kufuatia mashindano ya mwaka huu yaliyofanyika nchini Cameroon. Sababu za mashindano hayo ya mwaka huu kufanyika mwanzoni mwa mwaka ilikuwa ni hiyo hiyo ya mvua kubwa kunyesha katikati ya mwaka nchini Cameroon. Mwaka 2017, CAF ilitangaza uamuzi wa kuyahamisha mashindano hayo yawe yanachezwa katikati ya mwaka ili kuvirishisha vilabu vya Ulaya ambavyo haviko tayari kuwapa nafasi wachezaji wao muhimu wa Afrika wakashiriki kinyang'anyiro hicho katikati ya msimu.