Rais wa China, Xi Jinping leo amemwapisha kiongozi mpya wa Hong Kong huku akionya kuwa China haitavumilia upinzani wowote dhidi ya mamlaka yake katika eneo hili.
Kiongozi huyo ni wa kwanza mwanamke wa Hong Kong anayefahamika kwa jina la Carrie Lam.
Katika hotuba yake yenye maneno makali wakati wa kuadhimisha miaka 20 tangu koloni hilo la zamani la Uingereza kurejea kwa China, Jinping amesema juhudi zozote zinazofanywa na baadhi ya watu nchini kupinga mamlaka ya China hazitakubalika.
"Juhudi zozote zinazoweza kuhatarisha uhuru na mipaka ya China pamoja na usalama wake, ni sawa na kupambana na dola ya serikali kuu ya China na mamlaka ya sheria mama au kuitumia Hong Kong kuingiza mambo au shughuli za kuhujumu bara kitakuwa kitendo cha kuvuka mstari mwekundu,” amesisitiza.
Chini ya katiba ndogo ya Hong Kong , sheria ya msingi, jimbo hilo ambalo ni sehemu muhimu ya kiuchumi inahakikishiwa uhuru wake kwa takriban miaka 50 baada ya mwaka 1997.
Hong Kong ni jimbo maalumu la utawala ambalo linaongozwa chini ya utaratibu wa "nchi moja, mifumo miwili" unaoruhusu mamlaka makubwa ya ndani.
Jinping alikuwa akihutubia ukumbi uliojaa wageni waalikwa pamoja na watu mashuhuri wengi wao wakiwa ni waungaji mkono Serikali kuu mjini Beijing.