Romelu Lukaku arejea Inter Milan kwa mkopo baada ya kuagana na Chelsea

MSHAMBULIAJI matata raia wa Ubelgiji, Romelu Lukaku, 29, amerejea Inter Milan kwa mkopo, takriban mwaka mmoja baada ya kutua ugani Stamford Bridge kuvalia jezi za Chelsea.

Chelsea waliweka mezani kima cha Sh13.7 bilioni kwa ajili ya Lukaku mwishoni mwa msimu wa 2020-21. Hata hivyo, nyota huyo wa zamani wa Everton na Manchester United alisema “hafurahii maisha yake ugani Stamford Bridge na kwamba yalikuwa matamanio yake kurejea Italia.”

Inter wamekubali kuweka mezani kima cha Sh1.02 bilioni kufanikisha uhamisho wa Lukaku aliyewasaidia kutia kapuni taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo 2020-21.

Japo Chelsea hawakumwajibisha Lukaku mara nyingi mnamo 2021-22, mfumaji huyo alipachika wavuni mabao 15 katika mashindano yote.

Japo Lukaku alikuwa radhi kupunguziwa mshahara ili kufanikisha uhamisho wake hadi Inter kwa mkataba wa kudumu, hali tete ya kifedha kambini mwa Inter isingewazesha kumudu mshahara wa mshambuliaji huyo.

“Nimerudi nyumbani. Nina furaha tele kuingia upya katika sajili ya Inter,” akasema Lukaku.

Lukaku aliagana na Chelsea mnamo 2014 na kuyoyomea ugani Goodison Park kuchezea Everton baada ya kusajiliwa kwa mkataba wa miaka mitano uliogharimu Sh4 bilioni.

Hata hivyo, alitatizwa na visa vingi vya majeraha katika awamu ya pili ya kuhudumu kwake kambini mwa Chelsea huku akifungia kikosi hicho cha kocha Thomas Tuchel mabao matatu pekee katika mechi 15 za mwisho kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2021-22.

Chelsea walikamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya tatu huku Liverpool ikiwakomoa kwenye fainali ya Kombe la FA na League Cup kupitia mikwaju ya penalti.

Kwa upande wao, Inter waliambulia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Serie A mnamo 2021-22 baada ya kupigwa kumbo na AC Milan waliotawazwa mabingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10.

Kurejea kwa Lukaku kambini mwa Inter ni afueni tele kwa kikosi hicho kinachohusishwa pia na uwezekano wa kumsajili fowadi matata wa Juventus, Paulo Dybala.

Mkataba wa sasa kati ya Juventus na Dybala ambaye ni raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 28, utatamatika rasmi mwishoni mwa Juni 2022.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii