Polisi yavunja maandamano dhidi ya hali ngumu kiuchumi Ghana

Polisi nchini Ghana walilazimika kuingilia kati kuyavunja maandamano ya kupinga kupanda kwa bei za mafuta, kodi ya malipo ya kielektroniki na ushuru mwingine wakati nchi hiyo ikikumbwa na mtikisiko wa kiuchumi. Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi, risasi za mpira na maji ya moto dhidi ya waandamanaji wakati walipoondoka kwenye barabara za maandamano zilizoidhinishwa na mahakama. Watu kumi walikamatwa. Maandamano hayo ya siku mbili yaliandaliwa na shirika lenye nguvu nchini humo la Arise Ghana. Mfumko wa bei nchini Ghana umepanda hadi kiwango cha juu kabisa cha asilimia 27 kufuatia vita vya nchini Ukraine na janga la corona. Rais Nana Akufo-Addo yuko chini ya shinikizo kushughulikia kupanda kwa gharama ya maisha. Upinzani unasema kodi mpya ya serikali kwenye malipo ya kielektroniki itawaathiri watu wa kipato cha chini na biashara ndogo ndogo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii